KATIBU CCM Wilaya Songea Vijijini Ndugu Juma Nambaila amewataka wananchi kuunga mkono jitihada za serikali za utunzaji mazingira kwa kupanda miti katika maeneo mbalimbali.
Ameyasema hayo wakati wa zoezi la upandaji miti lililoudhuriwa na viongozi wa CCM, wataalamu na wanakijiji katika kituo cha afya Matimira.
“Tumedhamiria kurudisha uoto wa asili ambao ulipotea hivyo tumepanda miti isiyopungua 500 pamoja na wananchi waliojitokeza katika maeneo haya”, amesema Ndugu Nambaila.
Akizungumza Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea ambae pia ni Diwani wa Kata ya Matimira Mheshimiwa Menas Komba amewataka wananchi waache tabia ya kuchoma moto katika kipindi cha kuandaa mashamba kwaajili ya kilimo.
Hata hivyo ametoa wito kwa wananchi kuandika barua TFS ya kuomba miche ya miti ili waweze kupanda katika maeneo yao ya mashamba hivyo ametoa agizo kwa kila hekari ipandwe miti isiyopungua 15.
Kwaupande wake Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea Abdallah Mtuli amesema Halmashauri imejipanga kuendesha zoezi hili la upandaji miti kwa kupanda miti milioni 1,500,000 kwa mwaka.
Aidha, ameongeza kuwa upo mpango kabambe wa kuendeleza zoezi la upandaji miti ambapo shule tatu zilizopo Songea Vijijini zimepata ruzuku kutoka mfuko wa misitu wa Taifa ambapo kila shule itapata Shilingi milioni tano kwaajili ya kuandaa vitalu vya miti ambayo itasambazwa kwenye taasisi mbalimbali.
Zoezi la upandaji miti liliambatana na zoezi la usafi katika kituo cha afya Matimira.
Halmashauri ya Wilaya Songea
Anuani ya Posta: P.o.box 995, Songea
Simu: 2602320 / 2602176
Simu ya mkononi:
Barua pepe: dedsongea@songeadc.go.tz
Copyright ©2017 songeadc.go.tz. Haki imehifadhiwa