Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea, Bi. Elizabeth Mathias Gumbo, ametoa wito kwa wananchi na watumishi wote wa Halmashauri hiyo kujitokeza kwa wingi kushiriki katika zoezi la kupiga kura kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025.
Akizungumza ofisini kwake, Gumbo amesema kuwa maandalizi ya uchaguzi huo yanaendelea vizuri katika maeneo yote ya Wilaya ya Songea, huku akisisitiza umuhimu wa wananchi kutumia haki yao ya kikatiba kushiriki katika uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani
Ameeleza kuwa vituo vyote vya kupigia kura vitafunguliwa kuanzia saa 1:00 asubuhi hadi saa 10:00 jioni, na hivyo amewataka watumishi wa umma pamoja na wananchi wote kuhakikisha wanapanga muda wao mapema ili waweze kushiriki bila kisingizio. “Ni jukumu la kila mmoja wetu kuhakikisha tunatimiza wajibu huu wa kitaifa, kwani kura yako ndio sauti yako na ndiyo chachu ya mabadiliko tunayoyataka,” alisema.
Aidha, Mkurugenzi huyo amewahimiza wananchi kutambua kuwa kushiriki kupiga kura ni njia pekee ya kuchagua viongozi bora watakaosimamia maendeleo yao, Ameongeza kuwa mara nyingi wananchi hulalamika kuhusu viongozi wasio na ufanisi, lakini changamoto kubwa imekuwa ni watu wengi kutojitokeza kupiga kura licha ya kuwa ni haki yao ya msingi.
“Wananchi wengi wamekuwa wakisema wanahitaji viongozi bora, lakini hawajitokezi siku ya kupiga kura haki hii ni ya msingi na ni wajibu kwa kila mmoja kuhakikisha anaitumia kwa busara ili kuchagua viongozi watakaoharakisha maendeleo katika maeneo yetu,” alisisitiza.
Katika maandalizi ya kuelekea siku ya uchaguzi wananchi wanapaswa kutembelea vituo walivyojiandikisha ili kuthibitisha majina yao kwenye orodha ya wapiga kura, na pia kujionea karatasi ya mfano wa kupigia kura ambayo itaonesha namna sahihi ya kuweka alama ya kura. Hatua hiyo ni muhimu kwani itawasaidia wananchi kuepuka makosa yatakayoweza kusababisha kura zao kuharibika.
kwa mujibu wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi siku ya uchaguzi wanachi wanapaswa kufika vituoni wakiwa na kadi ya mpiga kura au kitambulisho cha taifa (NIDA) au, leseni ya udereva, au kitambulisho kingine chenye majina yanayofanana na yale waliyojiandikishia, kama uthibitisho wa utambulisho wao.
Katika hatua nyingine Halmashauri ya Wilaya ya Songea imekuwa mstari wa mbele katika kuhimiza uwajibikaji na ushirikishwaji wa wananchi katika shughuli za maendeleo, na uchaguzi ni mwendelezo wa juhudi hizo.
“Kura yako ni haki yako, Jitokeze kupiga kura" Kwa ujumla, kauli mbiu hii inahamasisha uzalendo, uwajibikaji na ushiriki wa wananchi katika mchakato wa demokrasia kwa njia ya amani. Inalenga kuondoa visingizio vya kutojitokeza kupiga kura na kuhimiza kila raia kuelewa kuwa maendeleo ya taifa yanaanza na kura yake.
Halmashauri ya Wilaya Songea
Anuani ya Posta: P.o.box 995, Songea
Simu: 2602320 / 2602176
Simu ya mkononi:
Barua pepe: dedsongea@songeadc.go.tz
Copyright ©2017 songeadc.go.tz. Haki imehifadhiwa