Katika kuendelea kuboresha upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wananchi, Serikali Kuu kupitia Wizara ya Afya imetoa zaidi ya shilingi milioni 891 kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya viwili ambavyo vitasaidia zaidi ya wananchi 23,800 walipo katika Kata ya Peramiho na Mpandangindo katika Halmashauri ya Wilaya ya Songea, mkoani Ruvuma.
Fedha hizo zinajumuisha kiasi cha shilingi milioni 641,627.778 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya cha Kata ya Peramiho, na shilingi milioni 250,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya cha Kata ya Mpandangindo.
Akizungumza baada ya mapokezi ya fedha hizo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea, Bi. Elizabeth Gumbo, alisema fedha hizo ni sehemu ya juhudi za serikali za kuhakikisha kila kata nchini inakuwa na kituo cha afya kinachotoa huduma muhimu kwa wananchi.
“Fedha hizi ni matokeo ya dhamira ya dhati ya serikali kuboresha huduma za afya vijijini. Tunashukuru Serikali Kuu kwa kuendelea kuiwezesha Halmashauri yetu kutekeleza miradi mikubwa yenye tija kwa wananchi,” alisema Bi. Gumbo.
Aliongeza kuwa miradi hiyo itatekelezwa kwa kuzingatia taratibu zote za manunuzi na usimamizi wa fedha za umma, ili kuhakikisha thamani halisi ya fedha inaonekana katika matokeo ya miradi.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Songea, Dr Geofrey Kihaule alisema kukamilika kwa ujenzi wa vituo hivyo viwili kutasaidia kupunguza msongamano wa wagonjwa katika Hospitali ya Wilaya ya Songea, na kuongeza kasi ya utoaji huduma hasa kwa akinamama wajawazito, watoto na wazee.
“Kupatikana kwa vituo hivi kutarahisisha upatikanaji wa huduma za afya ya uzazi, huduma za dharura, na maabara kwa wananchi waliokuwa wakitembea umbali mrefu kufuata matibabu,” alisema.
Wananchi wa kata hizo wamepokea kwa shangwe taarifa za fedha hizo, wakisema mradi huo utakuwa suluhisho la muda mrefu kwa changamoto ya upatikanaji wa huduma za afya karibu na makazi yao.
Bi. Janeth Mbawala, mkazi wa Kata ya Peramiho, alisema “Tumehangaika kwa muda mrefu kutafuta huduma za afya mbali, hasa akina mama wajawazito. Tunashukuru serikali kwa kutuona na kutuletea kituo cha afya karibu.”

Naye Bw. Sospeter Mlelwa wa Kata ya Mpandangindo alisema “Kwa kweli hii ni neema kubwa. Vituo hivi vitapunguza gharama na muda wa kusafiri, hasa wakati wa dharura.”
Kwa mujibu wa taarifa kutoka idara ya Afya ya Halmashauri ya Wilaya ya Songea, ujenzi wa vituo hivyo umeshaanza kutekelezwa huku wananchi wakihamasishwa kushiriki katika hatua za awali za ujenzi kwa nguvu kazi.
Kupitia utekelezaji wa miradi hii, Serikali inaendelea kuthibitisha azma yake ya kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma bora za afya kwa ukaribu, usawa na ubora unaostahili.
Halmashauri ya Wilaya Songea
Anuani ya Posta: P.o.box 995, Songea
Simu: 2602320 / 2602176
Simu ya mkononi:
Barua pepe: dedsongea@songeadc.go.tz
Copyright ©2017 songeadc.go.tz. Haki imehifadhiwa