KITENGO CHA USIMAMIZI WA TAKA NA USAFI WA MAZINGIRA
UTANGULIZI
Kitengo cha Usimamizi wa taka na usafi wa mazingira kinaendelea kutekeleza majukumu mbalimbali ya kila siku ya kusimamia shughuli za usafi na mazingira katika Halmashauri kwa lengo la kuimarisha usafi na utunzaji wa mazingira kuanzia ngazi ya kaya, kitongoji, kijiji, kata, wilaya, mkoa na Taifa kwa ujumla, kwa kuhamasisha jamii kushiriki kufanya usafi wa mazingira ili kuondokana na changamoto ya uzagaaji wa taka katika jamii hasa katika maeneo ya kaya, taasisi na maeneo ya biashara.
MAJUKUMU YA KITENGO
Kitengo cha Usafi na usimamizi wa taka kinatekeleza majukumu mbalimbali kwa kuzingatia Sheria ya afya ya jamii, Na. 1 ya mwaka 2009 na sheria ya utunzaji wa mazingira Na. 20 ya mwaka 2004 na mpango kazi wa taifa na hifadhi ya na usimamizi wa mazingira 2013- 2018, baadhi ya majukumu hayo ni kama yafuatayo;
Usafishaji na ukusanyaji wa taka kutoka kwenye majengo, maeneo ya wazi, barabara na mifereji ya kuondoa maji ya mvua.
Kuweka mifumo na miundombinu isiyoathilio afya na mazingira ya usimamizi wa taka kuanzia zinapozalishwa hadi zinapotupwa kwa kuzingatia utenganishaji, ukusanyaji na utupaji taka katika Madampo ya kisasa.
Kubuni mbinu za kupunguza taka na kusimamia utekelezaji wake ili kupunguza uchafu wa mazingira.
Kusimamia usafi katika mifereji ya kukusanya maji ya mvua na kuhakikisha inafanya kazi muda wote
Kufanya tafiti/uchunguzi kubaini aina ya taka zinazozalishwa kutoka katika masoko, makazi , maeneo ya biashara na taasisi.
Kuandaa na kusimamia miongozo ya kutenga maeneo kwa ajili ya kukusanya taka kwa muda.
Kutenga maeneo maalumu ya kuanzisha vituo vya kukusanya,kuchakata na kuhifadhi taka zitokanazo na vifaa vya umeme na elektronik, mafuta machafu na taka nyingine za sumu.
Kuweka vyombo vya kuhifadhia taka katika maeneo yote ya umma na kuhakikisha usafi wa maeneo hayo.
Kuainisha na kutenga maeneo maalumu na ya kutosha kwa ajili ya ujenzi wa Dampo za kisasa
Kuweka na kusimamia miongozo ya utupaji wa mwisho wa taka ngumu na uendeshaji wa Dampo za kisasa
Kuweka tozo ya usimamizi wa taka inayozingatia gharama halisi ya huduma katika ukusanyaji hadi utupaji katika madampo ya kisasa.
Kutoa amri za kuzuia utupaji ovyo wa taka wa aina zote katika fukwe, maeneo ya wazi, mito na mifereji ya maji ya mvua
HITIMISHO
Kitengo cha Usafi na Udhibiti wa taka imejipanga kuendelea kulipa umuhimu swala la usafi na kutia mkazo katika ngazi za chini ili iwe ni tabia katika jamii yetu watu kupenda kufanya usafi kwa ajili ya usalama wa afya na uboreshaji wa mazingira
Halmashauri ya Wilaya Songea
Anuani ya Posta: P.o.box 995, Songea
Simu: 2602320 / 2602176
Simu ya mkononi:
Barua pepe: dedsongea@songeadc.go.tz
Copyright ©2017 songeadc.go.tz. Haki imehifadhiwa