Leo Oktoba 23, 2025, Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Halmashauri ya Wilaya ya Songea kimetembelea eneo la ujenzi wa stendi ya mabasi katika Kijiji Cha Parangu inayotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) ambao upo hatua za mwisho za ukamilishaji wake, mradi unaogharimu zaidi ya shilingi milioni 500 hadi kukamilika kwake
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mratibu wa TASAF Halmashauri ya Wilaya ya Songea, Bi. Hosana Ngunge, amesema ujenzi wa stendi hiyo ni moja ya miradi mikubwa ya kimkakati inayotekelezwa na TASAF kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Songea. Alifafanua kuwa mradi huo unahusisha miundombinu muhimu kama matundu sita (6) ya vyoo, shedi nne (4), jengo la utawala, maduka 32 ya wafanyabiashara wadogo, pamoja na viunga vya maua vitakavyopamba eneo hilo.
“Kukamilika kwa mradi huu kutafungua milango ya kiuchumi kwa wananchi wa kata ya Parangu, Wananchi wataweza kufanya biashara zao kwa urahisi, wamiliki wa bodaboda na magari watapata fursa zaidi za kiuchumi, na suala la usafiri litakuwa jepesi kwani magari yatakuwa yanapaki moja kwa moja kijijini kwao,” alisema Bi. Ngunge.
Aliongeza kuwa mradi huo umezingatia vigezo vyote vya ubora na unatarajiwa kuwa kivutio kipya cha maendeleo kwa wananchi wa Parangu na maeneo jirani. Aidha, alisisitiza kuwa TASAF itaendelea kushirikiana na serikali za mitaa kuhakikisha miradi yote inayotekelezwa inaleta matokeo chanya kwa walengwa wake.
Kwa upande mwingine, wananchi wa Kata ya Parangu wameelezea furaha na shukrani zao kwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuona umuhimu wa kuwaletea maendeleo kupitia mradi huo wa stendi.

Mwenyekiti wa kijiji cha Parangu, Bwana Ditram Ngonyani, akizungumza kwa niaba ya wananchi, alisema:
“Kuwa na stendi katika kata yetu ni ndoto ambayo hatukuamini kama ingeweza kutimia. Tunamshukuru sana Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na TASAF kwa kutuona sisi wananchi wa Parangu. Mradi huu ukikamilika, wananchi wa kijiji chetu, kata na hata vijiji jirani watapata fursa nyingi za kiuchumi. Tunasema asante kwa Serikali yetu ya awamu ya sita kwa kuendelea kuleta maendeleo hadi ngazi ya kijiji.”

TASAF katika Halmashauri ya Wilaya ya Songea imekuwa ikitekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo yenye lengo la kuinua maisha ya wananchi, ikiwemo miradi ya afya, maji, ujenzi wa nyumba za watumishi, pamoja na utoaji wa ruzuku kwa kaya lengwa. Ujenzi wa stendi ya Parangu ni miongoni mwa miradi inayodhihirisha dhamira ya serikali katika kusogeza huduma karibu na wananchi na kuchochea ukuaji wa uchumi wa vijijini.
Kwa ujumla, mradi huu unatarajiwa kuwa chachu ya maendeleo kwa Kata ya Parangu, kwa kuongeza mzunguko wa fedha, kuboresha huduma za usafiri, kuongeza ajira, na kuwapa wananchi fursa mpya za kujiletea kipato. Kukamilika kwake kutakuwa ni hatua kubwa katika safari ya kuinua uchumi wa wananchi wa Songea Vijijini na kuongeza mapato ya Halmashauri kupitia shughuli mbalimbali zitakazofanyika katika eneo hilo la stendi.
Halmashauri ya Wilaya Songea
Anuani ya Posta: P.o.box 995, Songea
Simu: 2602320 / 2602176
Simu ya mkononi:
Barua pepe: dedsongea@songeadc.go.tz
Copyright ©2017 songeadc.go.tz. Haki imehifadhiwa