KAMATI ya fedha ikiongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea Mheshimiwa Menas Komba imefanya ziara ya ukaguzi wa miradi inayotekelezwa Songea vijijini.
Ziara hiyo ya ukaguzi imefanyika kuanzia tarehe 18 hadi tarehe 20 Januari 2023.
Ukaguzi huo umefanyika katika Kata ya Muhukuru ambapo kuna ujenzi wa Zahanati ya Matama ambayo ilianza kujengwa kwa nguvu za wananchi na michango kutoka kwenye Shirika la NSSF, mfuko wa Jimbo na Halmashauri kwa ushirikiano mkubwa wa Diwani Mhe. Manfred Mzuyu na Mbunge Mhe. Jenista Joakim Mhagama.
Akisoma taarifa Mtendaji wa Kata amesema ujenzi wa Zahanati hiyo ulianza kujengwa mwaka 2016 kwa nguvu za wananchi zenye thamani ya shilingi milioni5, michango ya wananchi shilingi milioni 9 na laki 4, Mheshimiwa Mbunge Shilingi milioni 1, Mfuko wa Jimbo shilingi milioni 5, shirika la NSSF lilichangia nondo na mifuko ya saruji na Halmashauri ya Wilaya ya Songea ilichangia shilingi milioni 60, kutoka mapato ya ndani, aidha ujenzi huo upo katika hatua za mwisho za ukamilishaji.
Vilevile ukaguzi umefanyika katika Kata ya Muhukuru ambapo kuna ujenzi wa shule ya msingi mpya ya Lizaboni, Halmashauri ilipokea fedha kiasi cha shilingi milioni 250 kwaajili ya kutekeleza mradi huo.
Akizungumza katika ukaguzi huo Mwenyekiti wa Halmashauri Mheshimiwa Komba amemuagiza Mtendaji Kata aandike barua TFS ya kuomba miti iliipandwe katika maeneo ya shule ili ikikamilika iwe na mazingira mazuri.
Pia ukaguzi umefanyika katika Kata ya Ndongosi kijiji cha Namatuhi katika shule ya msingi Muungano ambapo kuna ukamilishaji wa vyumba viwili vya madarasa yaliyoanza kujengwa kwa nguvu za wananchi pia Halmashauri imepeleka fedha kiasi cha shilingi Milioni 25 kutoka mapato ya ndani kwaajili ya kukamilisha ujenzi huo.
Mwisho, ukaguzi huo umefanyika Kata ya Mpandangindo katika shule ya msingi Liweta ambapo Halmashauri ilipokea fedha kiasi cha shilingi milioni100 kwaajili ya ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa, ukarabati wa vyumba saba vya madarasa na ujenzi wa matundu 20 ya vyoo.
Halmashauri ya Wilaya Songea
Anuani ya Posta: P.o.box 995, Songea
Simu: 2602320 / 2602176
Simu ya mkononi:
Barua pepe: dedsongea@songeadc.go.tz
Copyright ©2017 songeadc.go.tz. Haki imehifadhiwa