Mkuu wa Wilaya ya Songea, Mheshimiwa Kapenjama Ndile, ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Songea kwa hatua kubwa zinazochukuliwa kuboresha lishe katika jamii kwa kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2025/2026 (Julai–Septemba). Ametoa pongezi hizo leo, 17 Novemba 2025, wakati wa kikao cha lishe kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea.
Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Ndile ameisisitiza Halmashauri kuendeleza ari ya kuhakikisha makundi yote ndani ya jamii, ikiwemo watoto, kina mama wajawazito, vijana na wazee, yanapata lishe bora na stahiki. Amesema kuwa mafanikio ya lishe hayapaswi kuwa ya msimu, bali yawe endelevu ili Songea iendelee kuwa mfano bora katika juhudi za kupambana na utapiamlo nchini.
Aidha, amewataka wataalamu wa afya katika vituo mbalimbali kuimarisha ufuatiliaji wa taarifa za afya za watoto kwa kupima urefu, uzito na hali ya ukondefu mara kwa mara, hatua itakayochangia kubaini changamoto mapema na kuongeza ufanisi wa huduma za lishe.
Katika uwasilishaji wa taarifa ya utekelezaji wa mkataba wa afua za lishe, Bi. Joyce Sipira, Afisa Lishe wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea, alieleza kuwa hali ya lishe inaendelea kuimarika. Amesema kuwa shule nyingi sasa zinatoa chakula kwa wanafunzi, jambo ambalo limepunguza utoro wa wanafunzi shuleni.
Pia alibainisha kuwa idadi ya mashine za kusagia unga wenye virutubishi imeongezeka kutoka 5 hadi 8, hatua ambayo imeongeza upatikanaji wa unga ulioimarishwa kiafya katika jamii—hatua muhimu katika kupambana na udumavu na upungufu wa virutubisho mwilini.
Mhe. Ndile amewataka watendaji wa kata kuhakikisha mashine hizo mpya zinatangazwa na kufahamika katika vijiji vyote ili kuongeza matumizi na kuwafikia wananchi wengi zaidi. Katika hatua nyingine za kikao hicho, alikabidhi kibao maalum cha upimaji urefu wa watoto, lengo likiwa ni kuimarisha ufuatiliaji wa ukuaji na afya ya watoto katika ngazi ya jamii.
Halmashauri ya Wilaya Songea
Anuani ya Posta: P.o.box 995, Songea
Simu: 2602320 / 2602176
Simu ya mkononi:
Barua pepe: dedsongea@songeadc.go.tz
Copyright ©2017 songeadc.go.tz. Haki imehifadhiwa