Baraza la Madiwani ni chombo muhimu katika uendeshaji wa mamlaka za Serikali za Mitaa, Ndilo linalowakilisha wananchi katika ngazi ya Halmashauri, na kupitia Baraza hili, maamuzi mbalimbali ya kimkakati na kimaendeleo hupitishwa. Madiwani wanaounda baraza ni wale waliochaguliwa na wananchi pamoja na wale wa viti maalum.
Kitengo cha mwasiliano Serikalini, kilifika Ofisi ya Utumushi Halmashauri ya Wilaya ya Songea na kuongea na Mkuu wa Idara hiyo Ndg. Idd Kalingonji ambapo ameeleza Lengo kubwa la kuwa na Baraza la madiwani ni kurejeshwa kwa mhimili wa ngazi ya kiutawala katika Serikali za Mitaa ambapo huukamilisha muundo wa kimaamuzi na usimamizi katika Halmashauri.
Katika kipindi hiki ambacho Halmashauri huunda Baraza jipya la madiwani, kuna hatua muhimu zinazofanyika. Moja ya hatua hizo ni uchaguzi wa Mwenyekiti wa Halmashauri, ambaye ndiye kiongozi mkuu wa kisiasa katika baraza hilo, Mwenyekiti huyo huchaguliwa na madiwani wenyewe kupitia kikao cha kwanza cha baraza.
Katika mchakato wa kumpata mwenyekiti wa Halmashauri chama chochote cha siasa chenye mwakilishi kinaweza kupendekeza jina na kuliwasilisha kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri na kuweza kupigiwa kura na wajumbe wote.
Mwenyekiti wa Halmashauri ana majukumu ya kuongoza vikao vya Baraza, kusimamia utekelezaji wa maamuzi ya Baraza, kuhakikisha uwajibikaji, na kuwa kiunganishi kati ya Baraza na Wataalamu wa Halmashauri kwa pamoja, Baraza na menejimenti ya Halmashauri hushirikiana kupanga, kusimamia na kufuatilia miradi mbalimbali ya maendeleo katika maeneo yao.
Hivyo Baraza la Madiwani hufanya maamuzi ya mwisho kuhusu Halmashauri kama vile fedha, miradi, mipango na manunuzi ambapo hufanywa na kamati za kudumu kama vile Kamati ya Fedha Uongozi na Mipango, Kamati ya Uchumi, Ujenzi na Mazingira na Kamati ya Elimu, Afya na Maji. Pia kuna kamati zisizo za kudumu ambazo ni Kamati ya Maadili ya Madiwani na Kamati ya kudhibiti UKIMWI.
Kwa ujumla kikao cha baraza la madiwani kinahudhuriwa na madiwani wote wa kuchaguliwa na wa viti maalum, wakuu wa Idara na vitengo ( wataalam ), waalikwa kama vile Mkuu wa Mkoa na Katibu Tawala wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya na Katibu Tawala wa Wilaya, Ofisi ya Ufuatiliaji na usimamizi wa Serikali za Mitaa pia kamati ya ulinzi na usalama, viongozi wa vyama, wananchi na waandishi wa habari.

Katika kuelekea kuundwa kwa Baraza jipya la madiwani Ndug Idd Kalingonji Afisa Utumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea amesema Halmashauri imejipanga kikamilifu ikiwemo uandaaji wa taarifa za utendaji kazi wa Halmashauri kwa kipindi chote ambacho Baraza halikuwepo, kumuandaa Hakimu kwaajili ya Kiapo cha madiwani, kiapo cha Maadili na kiapo cha tamko mbele ya Mkurugenzi.
Pia Halmashauri imeandaa vitendea kazi kwaajili ya uchaguzi wa Mwenyekiti wa Halmashauri kama vile masanduku (Ballot paper) kuandaa mazingira rafiki ya kupigia kura, sare za wajumbe pamoja kuuandaa ukumbi.
Halmashauri ya Wilaya Songea
Anuani ya Posta: P.o.box 995, Songea
Simu: 2602320 / 2602176
Simu ya mkononi:
Barua pepe: dedsongea@songeadc.go.tz
Copyright ©2017 songeadc.go.tz. Haki imehifadhiwa