Idara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ya Halmashauri ya Wilaya ya Songea kupitia Kitengo cha Mifugo, ikiongozwa na Bw. Anton Sekumbo, imeendesha zoezi maalum la uhamasisho wa ulaji wa lishe bora kwa wanafunzi kwa kugawa maziwa mashuleni leo Novemba 27, 2025. Hatua hii ni sehemu ya jitihada endelevu za Serikali kuhakikisha watoto wanakuwa na afya bora na miili imara kupitia ulaji wa vyakula vyenye virutubishi muhimu.
Kwa mujibu wa wataalamu hao, Idara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ni miongoni mwa idara mtambuka zinazoshirikiana kwa karibu na Idara ya Afya katika kutekeleza masuala ya lishe kwa watoto, hususan wale wa umri wa shule. Kupitia ziara hiyo, wataalamu walipata nafasi ya kutoa elimu kwa wanafunzi na walimu juu ya faida za unywaji wa maziwa mara kwa mara, wakibainisha kuwa maziwa yana virutubishi muhimu vinavyosaidia ukuaji wa mwili, uimarishaji wa mifupa, kuongeza kinga ya mwili na kuchangia uwezo wa mwanafunzi kujifunza kwa ufanisi.

Aidha, program ya ugawaji wa maziwa mashuleni inalenga kuwajengea wanafunzi tabia ya kunywa maziwa si tu wakiwa shuleni bali pia majumbani, hivyo kuhakikisha afya njema inajengwa tangu utotoni. Zoezi hilo limefanyika katika shule za msingi Mapinduzi, Kilimani na Morogoro ambapo wanafunzi walionesha mwamko mkubwa na furaha wakati wa kupokea maziwa hayo. Elimu hiyo imeenda sambamba na kaulimbiu ya maadhimisho ya lishe ya mwaka 2025 isemayo: “Afya ni Mtaji Wako, Zingatia Unachokula.”
Vilevile, Kitengo cha Mifugo kimeendelea kutekeleza program mbalimbali za kuhamasisha ulaji wa vyakula vyenye protini, ambapo kitengo kiligawa sungura na mabanda ya kufugia sungura kwa shule mbalimbali kwa mwaka uliopita. Hatua hiyo ilikusudia kuchochea ufugaji wa sungura ili watoto na jamii kwa ujumla waweze kupata nyama, ambayo ni chanzo kizuri cha protini kwa ukuaji wa mwili.
Bw. Sekumbo alibainisha kuwa zoezi la leo ni mwendelezo wa kampeni pana ya lishe bora katika Halmashauri ya Wilaya ya Songea, na litaendelea kufanyika mara kwa mara kwa lengo la kupunguza udumavu na kuongeza uelewa wa jamii kuhusu ulaji sahihi. Alisisitiza kuwa lishe bora ni msingi wa maendeleo ya mtoto kiakili na kimwili, hivyo ni wajibu wa wazazi, walimu na jamii kwa ujumla kuhakikisha watoto wanapata chakula chenye ubora.
Halmashauri ya Wilaya ya Songea imeendelea kuwa mfano wa kuigwa katika kutekeleza program za lishe, ikilenga kuandaa kizazi chenye afya bora na uwezo wa kuchangia maendeleo ya Taifa.
Halmashauri ya Wilaya Songea
Anuani ya Posta: P.o.box 995, Songea
Simu: 2602320 / 2602176
Simu ya mkononi:
Barua pepe: dedsongea@songeadc.go.tz
Copyright ©2017 songeadc.go.tz. Haki imehifadhiwa