HALMASHAURI ya Wilaya ya Songea imefanya maadhimisho ya siku ya UKIMWI duniani ambayo yamefanyika katika Kata ya Mbinga Mhalule Desemba Moja.
Maadhimisho hayo yaliambatana na shughuli mbalimbali ikiwemo upimaji wa ugonjwa wa UKIMWI, Kifua Kikuu, Utoaji wa Chanjo ya Polio kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano na utoaji wa elimu ya Lishe.
Akizungumza katika maadhimisho hayo Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea Mheshimiwa Simoni Boniface Kapinga ambae amemwakilisha Mwenyekiti wa Halmashauri amesisitiza watu watumie muda mwingi kuangalia, kulinda na kusimamia afya zao.
Aidha amewashauri wananchi wawe na tabia ya kwenda kituo cha afya kupima afya mara kwa mara hii itakufanya uwe salama sana na kujiwekea uhakika wa kuishi maisha marefu.
‘’Kufa kwa ugonjwa wa UKIMWI kwa sasa ni ushamba yapo magonjwa ambayo sasa ni hatari Zaidi kuliko vile ambavyo sisi tunadhani, ugonjwa wa UKIMWI upo lakini serikali yetu ya Tanzania inatumia fedha nyingi sana kwaajili ya kutafuta dawa zinazosaidia kufubaza virusi vya UKIMWI hivyo nawasihi ndugu zangu tuwe tunapima afya zetu mara kwa mara na pale tunapogundulika tumepata Ugonjwa huu tuweze kuanza dawa mapema’’, amesisitiza Mheshimiwa Kapinga.
Nae Diwani Kata ya Mbinga Mhalule Mheshimiwa Nasri Nyoni amewataka wananchi wasijiziuke sana wachukue tahadhari UKIMWI upo na amewataka wataalamu waweze kutoa elimu mara kwa mara kwa wananchi juu ya ugonjwa huu.
Kwaupande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea Ndugu Neema Maghembe ambaye amewakilishwa na Mganga Mkuu wa Wilaya Geofrey Kihaule amesema Halmashauri imejipanga vizuri kwaajili ya kuimarisha usawa na kukemea unyanyapaaji kwa watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI.
‘’Ninawaomba wananchi muweze kutoa taarifa pale mnapokutana na vitendo vyovyote vya unyanyasaji, unyanyapaaji pamoja na udhalilishaji kwa watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI katika Ofisi ya Mkurugenzi ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa’’, amesema Dokta Kihaule.
Kauli Mbiu, Imarisha Usawa kwa Watu Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI.
Halmashauri ya Wilaya Songea
Anuani ya Posta: P.o.box 995, Songea
Simu: 2602320 / 2602176
Simu ya mkononi:
Barua pepe: dedsongea@songeadc.go.tz
Copyright ©2017 songeadc.go.tz. Haki imehifadhiwa