Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Mhe. Ruben Kwagila (MB), ametoa maelekezo 10 mahususi kwa wataalam na viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea, akisisitiza umuhimu wa nidhamu ya fedha, usimamizi madhubuti wa miradi ya maendeleo na matumizi sahihi ya mifumo ya Serikali.
Mhe. Kwagila alitoa maelekezo hayo Januari 10, 2026, wakati wa ziara ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo katika Shule ya Sekondari Amali Lundusi na Shule ya Sekondari Jenista Mhagama, sambamba na kupokea taarifa ya mapokezi ya wanafunzi wa Kidato cha Kwanza.
Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Mh. Prof. Riziki Shemdoe, Naibu Waziri alisema maelekezo hayo ni mwongozo wa jumla wa Wizara unaopaswa kuzingatiwa na Mamlaka zote za Serikali za Mitaa.
Kwanza, alisisitiza nidhamu katika makusanyo ya mapato ya ndani na matumizi ya fedha za umma, akisema “tukusanye kwa nidhamu na tutumie kwa nidhamu, ndipo tutakapopata matokeo chanya”. Aliwataka watumishi wote kuzingatia matumizi sahihi ya fedha za Serikali.

Pili, aliagiza miradi yote isimamiwe kikamilifu hadi kukamilika, akisisitiza kuwa bajeti zielekezwe kwanza katika kukamilisha miradi iliyopo kabla ya kuanzisha mipya. Alifafanua kuwa TAMISEMI imeigawa nchi katika kanda kwa kuzingatia gharama za ujenzi na malighafi, hivyo upangaji wa bajeti uzingatie uhalisia huo.
Tatu, aliagiza hoja zote za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) zijibiwe na maelekezo pamoja na ushauri wa Kamati zote za Bunge yatekelezwe kikamilifu ili hoja ziondoke kwenye vitabu vya Serikali.
Nne, alisisitiza matumizi ya mifumo ya Serikali akieleza kuwa TAMISEMI ni daraja la utekelezaji wa sera zote za Wizara. Alikataza ukusanyaji wa mapato nje ya mfumo wa TAUSI, matumizi ya fedha kupitia MUSE, na manunuzi kufanyika kupitia NEST, akisisitiza matumizi ya mifumo hiyo bila kukoma.
Tano, aliagiza fedha za ndani zipelekwe kwenye miradi kwa kuzingatia mipango na bajeti, sambamba na kulipa madeni ya wazabuni kwa wakati ili kuwawezesha kuendelea kutoa huduma bila kuyumbishwa kiuchumi.
Sita, alielekeza fedha za mikopo zitolewe kulingana na makusanyo halisi, mikopo itolewe kwa ukamilifu na isimamiwe kikamilifu ili fedha za Serikali zirejeshwe na wanufaika wengine waweze kunufaika.
Saba, aliagiza maeneo yote ya mali za Serikali ikiwemo ofisi za Halmashauri, shule, hospitali, vituo vya afya na zahanati yapimwe na kupatiwa hati miliki. Alisisitiza fedha zitengwe kwenye bajeti ili kuepuka migogoro ya ardhi isiyo ya lazima.
Nane, aliwataka watumishi kufanya kazi kwa bidii kila mmoja kwa ngazi yake, kuanzia vitongoji, vijiji, kata, tarafa hadi Halmashauri, akisisitiza kuwa kero za wananchi zisikilizwe na kutatuliwa kwa wakati.
Tisa, alisisitiza umuhimu wa ukaguzi wa mara kwa mara (routine inspection), akiwataka wataalam kuyafahamu majukumu yao, kuijua miradi na kuitembelea mara kwa mara ili kuongeza ufanisi wa utekelezaji.
Kumi, aliwataka watumishi kuzingatia Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2009, maadili ya utumishi na kanuni za mienendo (Code of Conduct), akisisitiza kuwa ni wajibu wa Maafisa Utumishi kusimamia sheria na maadili hayo.
Naibu Waziri alihitimisha kwa kuwataka wataalam na viongozi wote wa Serikali za Mitaa kuyatekeleza maelekezo hayo kwa vitendo ili kuhakikisha miradi ya maendeleo inawanufaisha wananchi na kuleta tija iliyokusudiwa.
Halmashauri ya Wilaya Songea
Anuani ya Posta: P.o.box 995, Songea
Simu: 2602320 / 2602176
Simu ya mkononi:
Barua pepe: dedsongea@songeadc.go.tz
Copyright ©2017 songeadc.go.tz. Haki imehifadhiwa