Leo January 09 kumefanyika kikao cha kujengeana uwezo kuhusu utekelezaji wa mpango wa Bima ya Afya kwa Wote katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea, kikao ambacho kililenga kuwajengea uelewa wa kina wadau mbalimbali ili kuhakikisha mpango huo unatekelezwa kwa ufanisi, uwazi na kuwafikia wananchi wote bila ubaguzi wa aina yoyote.

Kikao hicho kiliwakutanisha wadau kutoka sekta mbalimbali wakiwemo wataalam wa afya kutoka vituo vya kutolea huduma za afya, watendaji wa kata na vijiji, pamoja na maafisa kilimo wa kata, ambao ni nguzo muhimu katika kufikisha elimu sahihi kwa wananchi ngazi ya jamii.
Akifungua kikao hicho, Katibu Tawala wa Wilaya ya Songea Ndug Mtela Mwampamba alisisitiza kuwa uelewa wa wananchi ni msingi muhimu wa mafanikio ya utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote. Alieleza kuwa pale wananchi wanapoelewa kwa kina malengo, faida na utaratibu wa mpango huo, huwa rahisi kuikubali, kujiunga nayo na kuitumia ipasavyo katika kupata huduma za afya
Ndug Mtela Mwampamba aliongeza kuwa bima ya afya ni ngao muhimu inayowaepusha wananchi na gharama kubwa za matibabu pindi wanapokumbwa na maradhi, na hivyo kuwawezesha kuendelea kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji na maendeleo ya jamii.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea, Mhe George Ponera aliwataka wadau wote walioshiriki kikao hicho kwenda kuwa mabalozi wa elimu hiyo kwa wananchi katika maeneo yao ya kazi.
Alisisitiza kuwa Serikali imejipanga kikamilifu kuhakikisha kuwa huduma bora za afya zinapatikana kwa wananchi wote bila kujali hali zao za kiuchumi au kijamii, na kwamba utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote ni sehemu ya mkakati mpana wa Serikali wa kuboresha sekta ya afya nchini.

Alieleza zaidi kuwa jukumu la wadau hao ni kuhakikisha taarifa sahihi, za kweli na zilizo rahisi kueleweka zinawafikia wananchi, kwa kutumia lugha nyepesi na mifano halisi ya maisha ya kila siku, ili kuondoa hofu, dhana potofu na taarifa zisizo sahihi ambazo zimekuwa zikikwamisha mwitikio wa wananchi kujiunga na mpango wa bima ya Afya.
Halmashauri ya Wilaya Songea
Anuani ya Posta: P.o.box 995, Songea
Simu: 2602320 / 2602176
Simu ya mkononi:
Barua pepe: dedsongea@songeadc.go.tz
Copyright ©2017 songeadc.go.tz. Haki imehifadhiwa