Kama ilivyo siku ya wanawake, siku ya watoto, siku ya baba, siku ya vijana siku ya mtoto wa kike, leo ni siku ya wazee duniani, hivyo wananchi wote duniani tunaungana ili kuadhimisha siku ya wazee kwa namna tofauti tofauti.
Siku ya wazee Duniani ilianzishwa na Umoja wa Mataifa mwaka 1990, kuwa siku ya kuhimiza na kupinga dhana na imani potofu kuhusu Wazee na uzee na kutambua umuhimu na mchango wao katika jamii
Dunia ilianza kutambua uwepo wa Wazee mwaka 1959, hapa ndipo zilianza kutungwa sera mbalimbali ila kutokana na kuimalika kwa huduma za afya, miundombinu mbali mbali ya kuhudumia wazee ilifanyika Sensa mwaka 1950 na kupata wazee million 200 kote dunian. Ambapo mpaka 2050, tunategemea kuwa na wazee million 700, na kwa Afrika kutakua na wazee million 350 mpaka ifikapo 2050.
Kauli mbiu ya mwaka huu 2023 ni “UTHABITI WA WAZEE KWENYE DUNIA YENYE MABADILIKO” Siku hii Kitaifa itaadhimishwa Mkoani Geita October 06 2023, na kwa Wilaya ya Songea ilifanyika Kata ya Litisha kijiji cha Nakahuga September 29, 2023. Ambapo wao walikua na ujumbe usemao “UZEE NA KUZEEKA HAKUNA ATAYEKWEPA”
Katika maadhimisho hayo yaliyoratibiwa na Halmashauri ya wilaya ya Songea, mgeni Rasmi alikua Katibu Tawala wa Wilaya Mr. Mtela Mwampamba, aliyemuwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Songea. Ambapo pamoja na mambo mengine wazee walipewa Fursa ya kuonesha uwezo wao kwenye mambo mbalimbali kama vile , Kucheza mpira wa miguu, kukimbikiza kuku, kuvuta kamba nk, pamoja na hayo wazee walionesha mazao mbalimbali wanayoyalima kwa ajili ya chakula lakini pia biashara.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa wilaya, Katibu Tawala wa Wilaya ya Songea alisema “ niwaponge wazee wote kwa jinsi mlivyojitoa katika siku hii muhimu kwenu na kwetu, lakin kwa upekee niwaponge sana wakina babu na kina bibi walioshiriki katika michezo, kiukweli mmetupa somo sisi vijana. Niwapongeze pia kwa jinsi mnavyoshiriki kwenye kilimo, nimeona mazao yenu Mahindi, Mpunga, Ndizi na Maharagwe ama kwa hakika ninyi ni wazee wa mfano na ndio maana Mhe Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ameamua kuwekeza nguvu kubwa katika kuhakikisha vijiji vyote vinapata Mbolea ya Ruzuku tena kwa Bei nafuu”
Aidha wazee pia walishauriwa kuwekeza nguvu yao kwenye kujishughulisha katika mambo mbalimbali ili kuepukana na magonjwa nyemelezi ambayo yamekua yakiwasumbua wazee wengi na kupelekea vifo vingi kwa wazee.
Dr. Geofrey Kihaule Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea alisema “ tunapaswa kuangalia magonjwa yanayoambatana na uzee kwa kuliangalia hilo ndio mana sisi kama serikali tumeamua kusimamia zoezi la upimaji wa afya kwa wazee wetu wote leo ili wajue matatizo yao na wapewe tiba. Lakini pia tunatambua wazee wanalishe duni ambayo hupelekea kupata magonjwa yanayotokana na changamoto ya lishe. Kutokufanya mazoezi kunachangia kinga za mwili kushuka”
Kwa upande wake Bi. Zawadi Nyoni aliyemuwakilisha Mkurugenzi mtendajiwa halmashauri, aliwashukuru wazee wote kwa kuitikia wito, na kujito kwa ajili ya siku hiyo muhimu, wadau mbalimbali waliochangia zoezi hilo kwenda kama lilivyopangwa na uongozi wa wilaya na serikali kuu kwa kusimamia vema jambo hili na kuona umuhimu wa wazee.
Halmashauri ya Wilaya Songea
Anuani ya Posta: P.o.box 995, Songea
Simu: 2602320 / 2602176
Simu ya mkononi:
Barua pepe: dedsongea@songeadc.go.tz
Copyright ©2017 songeadc.go.tz. Haki imehifadhiwa