Serikali kupitia Mfuko wa kunusuru kaya masikini Nchini imetoa kiasi cha shilingi zaidi ya milioni 155 kwa ajili ya kujenga soko la kisasa katika Kijiji cha Peramiho (B) kilichopo Kata ya Peramiho Halmashauri ya Wilaya ya Songea mkoani Ruvuma
Mratibu wa TASAF wa Halmashauri hiyo Hosana Ngunge amesema fedha hizo tayari zimeshaingizwa kwenye akaunti ya Kijiji kwa lengo la kuanza ujenzi wa soko hilo ambalo utekelezaji wake utachukua muda wa miezi sita kufuatana na miongozo iliyotolewa na Serikali.
Ngunge ameitaja miundombinu ambayo itakayoanza kujengwa katika soko hilo kuwa ni choo matundu manne,vizimba na ghuba la taka.
Ngunge amesema TASAF kipindi cha pili awamu ya tatu imejikita zaidi katika kukuza uchumi wa kaya ambazo ni masikini sana kwa njia ya kutoa ruzuku ya fedha,ruzuku ya masharti,kuunda vikundi ambavyo vinajiwekea akiba na kukopeshana kwa riba nafuu kupitia fedha za ruzuku wanazozipata na ajira za muda mfupi.
Kwa upande wake Diwani wa Kata hiyo Mhe Nikolaus Lutengano amewashukuru wananchi ambao wametoa maeneo yao kwahiari kwa nia ya kupisha ujenzi wa soko,na amehaidi kutoa ushirikiano wa kufuatilia na kusimamia utekelezaji wa mradi hadi unakamilika na wananchi wake wanaanza kunufaika na huduma.
Ameipongeza serikali na viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea kwa kusimamia na kufuatilia upatikanaji wa fedha hizo ambazo zinakwenda kutatua changamoto iliyokuwa ikiwakabili wananchi wa kijiji cha peramiho(B) cha kutokuwa na soko la kisasa.
Awali akizundua ujenzi wa soko hilo Mkuu wa Wilaya ya Songea Pololet Mgema ametoa rai kwa viongozi kusimamia mradi kwa umakini mkubwa na kuhakikisha mradi unatekelezwa vizuri na unatoa matunda chanya.
“Nataka soko lijengwe kwa miezi mitatu badala ya miezi sita ,“amesisitiza Mgema.
Mgema ametaka soko hilo lijengwe kwa muda wa miezi mitatu kwa lengo la kuwasaidia baadhi ya wafanyabiashara kulinda na kutunza mitaji yao sanjari na kutoa fursa kwa wananchi kuanza kupata huduma za soko.
Ametoa wito kwa wananchi kuunga mkono jitihada za Serikali ambayo imekuwa ikitoa fedha nyingi katika utekeleza wa miradi mbalimbali ya maendeleo kama vile Afya,Maji,Barabara,Elimu na miundombinu mingine,kujitoa kwenye kusimamia na kujitolea nguvu zao wanapotakiwa katika kufanikisha lengo.
Ujenzi wa soko hilo la kisasa katika kijiji hicho unakwenda kutatua kero na changamoto za soko la uhakika na kuongeza mapato ya Halmashauri kupitia tozo na ushuru.
Imeandikwa na
Jacquelen Clavery
Songea DC
Halmashauri ya Wilaya Songea
Anuani ya Posta: P.o.box 995, Songea
Simu: 2602320 / 2602176
Simu ya mkononi:
Barua pepe: dedsongea@songeadc.go.tz
Copyright ©2017 songeadc.go.tz. Haki imehifadhiwa