MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea Ndugu Neema Maghembe ameongoza zoezi la ugawaji vishikwambi kwa walimu wa shule za msingi na sekondari zilizopo Songea vijijini.
Zoezi hilo limefanyika tarehe 12 Januari katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri Lundusi-Peramiho ambapo vishikwambi 577 vimegawiwa kati ya 807 vilivyohitajika hivyo kuna upungufu wa vishikwambi 230 ili kukidhi mahitaji ya walimu wote.
Akizungumza katika zoezi hilo amewataka walimu kutunza zana hizo za kazi (vishikwambi) pamoja na maelekezo yote yaliyotolewa kutoka kwenye muongozo juu ya utunzaji na utumiaji ufuatwe.
“Tunakila sababu ya kuishukuru serikali yetu ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais wetu Dkt Samia Suluhu Hassan pamoja na Mbunge wetu wa Jimbo la Peramiho Mheshimiwa Jenista Joakim Mhagama kwa kuendelea kutuboreshea miundombinu katika sekta ya elimu”, amesema Ndugu Neema.
Akisoma muongozo wa vishikwambi Afisa Rasilimali watu na Utawala Ndugu Hashimu Lugome amesema vishikwambi ni mali ya serikali hivyo vitasimamiwa kwa mujibu wa sheria na kanuni ya manunuzi ya umma.
Ameongeza kuwa mwalimu aliyepokea kishikwambi endapo atastaafu, ataacha kazi, atafukuzwa au kufariki mali hiyo inapaswa irejeshwe serikalini.
‘’Vishikwambi hivyo vimeletwa kwaajili ya matumizi ya kujifunzia na kufundishia kwa walimu wa shule za msingi na sekondari na si kwa matumizi mengine hivyo mkishavipokea mkatekeleze kama masharti yalivyoelekezwa’’, amesisitiza Ndugu Lugome.
Akizungumza Afisa Elimu Msingi Bi Lucy Mbolu amewasisitiza walimu vishikwambi hivyo vitumike katika mambo ya msingi kama kutumiana maswali, kapakua vitu mbalimbali vya ufundishaji mtandaoni lengo ni kuongeza ufaulu katika shule za msingi na sekondari.
Nae Afisa Elimu Sekondari Bi Bumi Kasege amewaasa walimu wazingatie usalama katika utunzaji wa vishikwambi hivyo pia amewaelekeza walimu waliopata vishikwambi hivyo waweze kushirikiana na wengine ambao hawajapata ili waendelee kuboresha ujifunzaji na ufundishaji shuleni.
Halmashauri ya Wilaya Songea
Anuani ya Posta: P.o.box 995, Songea
Simu: 2602320 / 2602176
Simu ya mkononi:
Barua pepe: dedsongea@songeadc.go.tz
Copyright ©2017 songeadc.go.tz. Haki imehifadhiwa