Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashuri ya Wilaya ya Songea Ndg Neema M Maghembe amewasisitiza Maafisa kilimo wote ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Songea kuhakikisha wanapima afya ya udongo kwa wakulima bila kudai gharama zozote.
Ameyasema hayo wakati akifunga mafunzo ya upimaji wa afya ya udongo yaliyofanyika 10/11/2023 katika ukumbi wa ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Songea ambapo amewataka maafisa kilimo hao mpaka kufikia mwezi disemba wawe wamefikia malengo fulani katika kuwahudumia wakulima kupitia mafunzo hayo. Amesema
" Wataalamu wenzangu natambua sana mchango wenu kwenye vijiji mpaka kwenye Kata zenu na inafahamika kwamba Kilimo ndio uti wa mgongo wa mapato ya Halmashauri yetu hivyo kupitia Elimu hii niwaombe ikawe chachu ya kuongeza uzalishaji wa mazao ya Kilimo".
Lakini niwasisitize kitu kimoja mwongozo unatutaka tufanye shughuli hizi za upimaji wa afya ya udongo pasipo kumtoza mkukima gharama zozote nami nawaagiza nisisikie mkulima hajapimiwa udongo eti kwasababu hakuwa na fedha za kumuwezesha Afisa Kilimo kufanya hiyo shughuli hapo hatutaelewana, kwahiyo Mimi niwaombe tu ndugu zangu tukafanye kazi kadri ya miongozo tunayopewa". Alisema Ndg Neema M Maghembe Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashuri ya Wilaya ya Songea.
Nae Frank Sungau Afisa Kilimo wa makao makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Songea amesisitiza suala hilo na kutoa semina elekezi jinsi ya kuchukua sampuli ya udongo katika shamba la mkulima ambapo pia amewataka Maafisa kilimo hao kuhakikisha wanakwenda kwenye maeneo husika ya wakulima kuchukua taarifa zao. Amesema
"Pamoja na kufanya vipimo hivi bila gharama zozote basi niwaombe tuwe waaminifu katika kutoa taarifa za wakulima zilizo sahihi ikiwa ni pamoja na kufika shambani kwa mkulima na kuchukua sampuli ya udongo na kuja Kupima na sio umekaa kijiweni unajitungia taarifa za mkulima".
Baada ya mkulima kufanyiwa vipimo vya afya ya udongo wa shamba lake atapatiwa cheti cha uthibitisho wa kwamba shamba lake limefanyiwa vipimo vya afya ya udongo na cheti hicho pia atapatiwa bure bila gharama zozote na Kisha atashauriwa ni aina gani ya mbolea anatakiwa kutumia kutokana na vipimo vya udongo wa shamba lake.
Halmashauri ya Wilaya Songea
Anuani ya Posta: P.o.box 995, Songea
Simu: 2602320 / 2602176
Simu ya mkononi:
Barua pepe: dedsongea@songeadc.go.tz
Copyright ©2017 songeadc.go.tz. Haki imehifadhiwa