Halmashauri ya Wilaya ya Songea kupitia Idara ya Maendeleo ya Jamii imetoa mikopo yenye jumla ya Tsh 249,014,000 kwa vikundi 28 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, fedha ambazo zinatokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
Akizungumza wakati wa kutoa elimu juu ya matumizi sahihi ya mikopo hiyo, Afisa Maendeleo ya Jamii wa Wilaya ya Songea, Bi Zawadi Nyoni, alieleza kuwa Halmashauri ilipokea jumla ya maombi kutoka kwa vikundi 62, lakini ni vikundi 28 pekee ndivyo vilivyokidhi vigezo na kupatiwa mikopo hiyo. Alibainisha kuwa kati ya fedha hizo, Tsh milioni 116.5 zilitolewa kwa vikundi 15 vya wanawake, Tsh milioni 116.5 kwa vikundi 7 vya vijana, na Tsh 14,014,000 kwa vikundi 6 vya watu wenye ulemavu.
Bi Zawadi alieleza kuwa fedha hizo tayari zimeingizwa kwenye akaunti za vikundi husika na kusisitiza kuwa ni wajibu wa wanufaika kutumia mikopo hiyo kwa malengo yaliyokusudiwa ili kujiwezesha kuleta maendeleo ya kweli kwa jamii na kurahisisha urejeshaji wake kwa wakati.
Katika mafunzo hayo, wanachama wa vikundi walielimishwa kuhusu umuhimu wa kuweka kumbukumbu sahihi za matumizi ya fedha, kubuni miradi yenye tija, na kuwa na mpango wa marejesho endelevu ili kuhakikisha mzunguko wa mikopo hiyo unawanufaisha wananchi wengi zaidi katika siku zijazo.
Idara ya Maendeleo ya Jamii imejipanga kuendelea kutoa elimu kwa vikundi mbalimbali kabla na baada ya utoaji wa mikopo ili kuongeza ufanisi wa matumizi ya fedha hizo na kuboresha hali ya maisha ya wananchi wa Wilaya ya Songea, hasa makundi maalum yanayolengwa na mikopo hiyo.
Halmashauri ya Wilaya Songea
Anuani ya Posta: P.o.box 995, Songea
Simu: 2602320 / 2602176
Simu ya mkononi:
Barua pepe: dedsongea@songeadc.go.tz
Copyright ©2017 songeadc.go.tz. Haki imehifadhiwa