UJENZI WA HOSTELI
Halmashauri ya wilaya ya Songea, mkoani Ruvuma imekamilisha ujenzi wa hosteli katika shule ya Sekondari Barabarani kwa asilimia 85 kupitia mpango wa lipa kutokana na matokeo(EP4R)
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea Bw Simoni Bulenganija amesema mpango wa EP4R utasaidia wanafunzi kutojiingiza katika vishawishi ambavyo vitakavyopelekea kupata mimba na utoro na kukatisha masomo.
Amesema Serikali kupitia Halmashauri imejipanga kuhakikisha mazingira ya kujifunzia na kufundishia yanaboreshwa kwa kujenga hosteli kwa ajili ya wanafunzi wa kike na wavulana wanaoishi mbali na mazingira shule kazi ambayo inaendelea kwa sasa katika Halmashauri hiyo.
Amesema hosteli hiyo itakapokamilika itapunguza adha kubwa kwa wanafunzi ya kupanga vyumba kwa ajili ya kulala. Aidha hosteli hiyo inauwezo wa kutoa huduma ya malazi kwa wanafunzi 170 kati yao wasichana 85 na wavulana 85.
Bw Bulenganija amesema kwa sasa ujenzi huo umekamilika kwa asilimia 85 huku akiwashukuru wananchi wa kijiji hicho cha Muhukuru Barabarani kwa kuonyesha ushirikiano katika kipindi cha ujenzi wa hosteli kwa ulinzi shirikishi.
Alisema asilimia 15 zilizobaki kwa ajili ya kukamilisha ujenzi huo pamoja na kazi za kupachika milango, madirisha na kupaka rangi , kazi hiyo itakapo kamilika hosteli hiyo itaanza kutoa huduma mara moja kwa wanafunzi ambao kwa sasa wanakaa nje ya mazingira ya shule kwa kupanga nyumba .
Naye diwani wa kata ya Muhukuru katika Halmashauri ya Songea Manufred Mzuyu alipohojiwa na mwandishi wa habari hizi alisema mradi huo ulitakiwa kukamilika mwezi Machi 30 mwaka huu lakini anashangaa hadi hivi sasa mradi huo haujakamilika na wanafunzi wanaendelea kuishi kwa kupanga nyumba za wenyeji kitu ambacho alidai ni hatari kwa wasichana kutokana na vishawishi vya kupata mimba na utoro.
Kwa upande wake Mhandisi wa halmashauri ya wilaya ya Songea Bw Frank Hosea alisema ujenzi huo wa hosteli umechelewa kukamilika kwa wakati kutokana na jiografia ya hamlashauri hiyo katika kipindi cha masika miundo mbinu hasa barabara zilikuwa hazipitiki na kushindwa kusafirisha vifaa vya viwandani kufika katika eneo la mradi.Mradi huo umegharimu jumla ya shilingi milioni 150 hadi kukamilika kwake.
JACQUELEN CLAVERY-TEHEMA
Halmashauri ya Wilaya Songea
Anuani ya Posta: P.o.box 995, Songea
Simu: 2602320 / 2602176
Simu ya mkononi:
Barua pepe: dedsongea@songeadc.go.tz
Copyright ©2017 songeadc.go.tz. Haki imehifadhiwa