MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea Ndugu Neema Maghembe anautaarifu Umma kuwa, Halmashauri imepokea fedha kiasi cha shilingi milioni 55,824,000 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa mawili ya Elimu ya Awali ya mfano katika shule ya msingi Ngahokora.
Fedha hizo zimetolewa na Ofisi ya Rais- TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ikiwa ni fedha za utekelezaji wa mradi wa kuimarisha Stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) kwa Elimu ya Msingi kwa awamu ya pili (GPE-LANES II).
Amesema utekelezaji wa mradi huo utahusisha ujenzi wa madarasa mawili (02), ujenzi wa matundu manne (04) ya vyoo vya kawaida na matundu mawili (02) ya vyoo vya wanafunzi wenye mahitaji maalumu, ununuzi au utengenezaji wa samani za ndani viti na meza, ununuzi wa matanki mawili (02), mikeka mitano (05), shubaka, bembea (michezo ya wanafunzi), maandalizi ya viwanja vya michezo, ununuzi wa kizima moto, kutengeneza mfereji wa maji pamoja na kigundua moto.
Ameongeza kuwa Mradi wa kuimarisha Stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) kwa Elimu ya Msingi Awamu ya Pili (GPE-LANES II) ni msaada, hivyo haupaswi kulipa kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).
Vilevile Mkurugenzi Neema amebainisha kuwa kulingana na maelekezo ya Serikali, mradi huo utatekelezwa kwa kutumia Force Account na unatakiwa kukamilika kabla au ifikapo tarehe 15 Juni, 2023.
Aidha, Uongozi wa Halmashauri unatoa shukrani kwa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan na Mbunge wa Jimbo la Peramiho Mheshimiwa Jenista Joakim Mhagama kwa kuleta fedha kwa ajili ya kuboresha huduma za kijamii hususani Elimu.
Halmashauri ya Wilaya Songea
Anuani ya Posta: P.o.box 995, Songea
Simu: 2602320 / 2602176
Simu ya mkononi:
Barua pepe: dedsongea@songeadc.go.tz
Copyright ©2017 songeadc.go.tz. Haki imehifadhiwa