HALMASHAURI ya Wilaya ya Songea imepokea fedha kiasi cha Shilingi Milioni 100 kutoka Serikali Kuu kwaajili ya kutekeleza mradi wa ujenzi na ukarabati wa miundombinu katika Shule ya msingi Liweta.
Hayo yamebainishwa na Afisa Elimu Msingi Lucy Mbolu katika kikao cha kutambulisha mradi kwa wananchi wa Kata ya Mpandangindo kijiji cha Liweta ambacho kiliudhuriwa na Viongozi wa Kata, Kijiji, Wataalamu na kamati za ujenzi.
Akizungumza katika kikao hicho amesema katika Milioni 100 Milioni 40 zitatumika kujenga madarasa mawili mapya, Milioni 25 zitatumika kujenga matundu 20 ya vyoo na Milioni 35 zitatumika katika kukarabati miundombinu.
‘’Nawaomba kamati zote ambazo zimechaguliwa muwe na ushirikiano baina yenu, Viongozi na wananchi muende mkawe mabalozi katika kuutangaza huu mradi pamoja na kuwasisitiza wananchi wawajibike katika ujenzi huu pale ambapo zinahitajika nguvu za wananchi basi waweze kujitoa na kujituma ili kuhakikisha mradi unakwenda vizuri’’, amesisitiza Afisa Elimu Lucy.
Vilevile Afisa elimu Lucy amesema Serikali imedhamiria kuboresha sekta ya elimu hivyo mradi huu inatakiwa kuonyesha thamani ya fedha iliyokuja kwa kuzingatia viwango na vigezo vilivyowekwa na serikali pia kuwa na uzalendo katika kuusimamia na kuulinda mradi huu.
Kwaupande wake Diwani wa Kata ya Mpandangindo Mheshimiwa Gothard Haule amesisitiza kwa wanakamati na Viongozi wa kata na Kijiji kwamba maelekezo yote yaliyotelewa na wataalamu yafanyiwe kazi hivyo amewataka kuwa wasimamizi wazuri wa mradi ili uwe na thamani halisi na fedha iliyopokelewa.
Aidha ameishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan na Mbunge wa Jimbo la Peramiho Mheshimiwa Jenista Joakim Mhagama kwa kuleta fedha kwaajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali na kuendelea kuboresha sekta ya elimu.
Halmashauri ya Wilaya Songea
Anuani ya Posta: P.o.box 995, Songea
Simu: 2602320 / 2602176
Simu ya mkononi:
Barua pepe: dedsongea@songeadc.go.tz
Copyright ©2017 songeadc.go.tz. Haki imehifadhiwa