HALMASHAURI ya Wilaya ya Songea imepokea shilingi Milioni 250 kutoka Serikali Kuu kuanza utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa shule ya msingi Lizaboni ambayo inajengwa katika kijiji cha Muhukuru Barabarani.
Hayo yamethibitishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea Ndugu Neema Maghembe ambae amewakilishwa na Afisa Elimu Sothery Nchimbi wakati wa kikao na wananchi wa kijiji cha muhukuru Barabarani.
Hata hivyo amesema lengo la kikao hiko ni kutambulisha mradi kwa wananchi, kuunda kamati ambazo zitasimamia zoezi zima la utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa shule pamoja na kupima maeneo.
‘’Nawaomba kamati zote ambazo zimechaguliwa tuhamasike, tujihamasishe na tuwahamasishe wananchi wengine pale ambapo inahitaji kujitoa hasa katika kulinda vifaa tujitoe kwelikweli ili ujenzi wetu uweze kwenda vizuri na kukamilika kwa wakati’’, amesisitiza Afisa Elimu Nchimbi.
Ametoa rai kwa wananchi wawajibike katika ujenzi huu pale ambapo zinahitajika nguvu za wananchi basi waweze kujitoa na kujituma ili kuhakikisha mradi unakwenda vizuri.
Kwaupande wake mwenyekiti wa Kitongoji Ndugu Semblini Komba amewashukuru wajumbe kwa elimu waliyoitoa na ameahidi yote yaliyosemwa watayafuata na kuwa kipaumbele katika kuwaelekeza wengine.
Wakizungumza wananchi wa kijiji cha Mhukuru barabarani wameishukuru Serikali ya awamu ya sita ikiongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Mbuge wa Jimbo la Peramiho Mheshimiwa Jenista Joakim Mhagama.
Pia wamemshukuru Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea Mheshimiwa Menace Komba, Mkurugenzi Mtendaji Ndugu Neema Maghembe, Diwani wa kata ya Muhukuru Barabarani Mheshimiwa Manfred Mzuyu pamoja na Watendaji wote kwa kuweza kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili.
Imeandaliwa na Bahati Nyoni,
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini.
Septemba 15, 2022.
Halmashauri ya Wilaya Songea
Anuani ya Posta: P.o.box 995, Songea
Simu: 2602320 / 2602176
Simu ya mkononi:
Barua pepe: dedsongea@songeadc.go.tz
Copyright ©2017 songeadc.go.tz. Haki imehifadhiwa