MWENYEKITI Wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya Ndugu Thomas Masolwa amewataka wataalamu wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea kuendeleza uwajibikaji katika Idara zao.
Ameyasema hayo wakati akizungumza na wakuu wa Idara katika ukumbi wa mikutano Lundusi- Peramiho akiambatana na Katibu wa Chama, Katibu mwenezi wa Chama, Mwenyekiti Jumuiya ya wazazi Songea Vijijini, Mjumbe wa Kamati ya Siasa Wilaya na Katibu wa Umoja wa Vijana.
Lengo lilikua ni kuja kusalimiana na kuja kutambulisha Viongozi kwa watumishi wa Halmashauri ambao walichaguliwa katika uchaguzi uliofanyika hivi karibuni.
Ndugu Thomas amewasisitiza watumishi kuwa na Umoja na mahusiano mazuri baina yao na watu wanaowaongoza ili Halmashauri iweze kwenda mbele Zaidi kwa maendeleo.
Aidha amewapongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan na Mbunge wa Jimbo la Peramiho Mheshimiwa Jenista Joakim Mhagama kwa kufanya mambo makubwa yanayojenga Halmashauri na kutekeleza miradi mbalimbali.
Pia amewapongeza Baraza la Madiwani wakiongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri Mheshimiwa Menas Komba, Mkurugenzi Mtendaji Ndugu Neema Maghembe pamoja na timu ya wataalamu kwa usimamizi mzuri wa miradi inayotekelezwa.
‘’Napenda kutoa rai kwenu tuendelee kuchapa kazi kwa kushirikiana na Viongozi wa Kata na Kijiji jitumeni Zaidi katika kutekeleza na kusimamia vizuri miradi pia kuwa na tabia ya kusikiliza changamoto za wananchi na kuwapa majibu ambayo yanaenda kutatua changamoto zao hii italeta heshima kubwa katika Halmashauri yetu’’, amesisitiza Ndugu Thomas.
Kwaupande wake Mwenyekiti wa Halmashauri Mheshimiwa Menas Komba amemshukuru Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi kwa maneno mazuri ya kutia moyo na kuahidi maelekezo yote aliyoyatoa yamezingatiwa.
‘’Maelekezo yote uliyoyatoa tumeyazingatia hatutakuangusha na tunakuahidi tunaenda kuongeza weledi na usimamizi mzuri na majibu yote tunaenda kuyaonesha kwa vitendo’’, amesema Mhe.Menas.
Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea Ndugu Neema Mghembe amewapongeza Viongozi wote wa Chama waliochaguliwa katika uchaguzi uliofanyika ameahidi kutekeleza yote yaliyosemwa na kuwapa ushirikiano katika kuhakikisha kwamba Halmashauri Hairudi nyuma.
Halmashauri ya Wilaya Songea
Anuani ya Posta: P.o.box 995, Songea
Simu: 2602320 / 2602176
Simu ya mkononi:
Barua pepe: dedsongea@songeadc.go.tz
Copyright ©2017 songeadc.go.tz. Haki imehifadhiwa