Mkuu wa Wilaya ya Songea, Mhe. Kapenjama Ndile, amewapongeza Wataalam na Watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea pamoja kwa kazi nzuri ya kusimamia na kuboresha vizuri utekelezaji wa shughuli za lishe katika maeneo yao.
Akizungumza katika kikao cha lishe Cha robo ya tatu 2024/2025 kilichofanyika leo katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea, Mheshimiwa Ndile alisema:“Halmashauri hii inafanya vizuri sana katika kuimarisha lishe bora kwa watoto. Pongezi nyingi kwenu kwa kazi nzuri mnayoifanya kwa ustawi wa jamii yetu.”
Hata hivyo, Mkuu huyo wa Wilaya aliwataka watendaji kuongeza juhudi zaidi katika kata ambazo bado zina viwango vya chini vya lishe “Ni muhimu kuongeza nguvu na ubunifu katika kata ambazo hali ya lishe bado haijaridhisha, ili kuhakikisha kila mtoto anapata lishe bora bila kujali eneo analotoka,” alisisitiza.
Aidha, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea, Bi Elizabeth Gumbo, alitoa pongezi kwa watendaji wa kata kwa usimamizi wao mzuri wa masuala ya lishe.
“Napenda kuwapongeza sana kwa jitihada zenu. Kupitia kazi yenu, Halmashauri yetu imeendelea kuwa katika nafasi nzuri katika hali ya lishe,” alisema Bi. Gumbo.
Katika kikao hicho, Afisa Lishe wa Halmashauri, Bi Joyce Sipira, aliwasilisha taarifa ya hali ya lishe kwa kipindi cha robo ya tatu ya mwaka 2024/2025 ambapo pamoja na mambo mengine alielezea mafanikio yaliyopatikana ambayo ni pamoja na kuwajengea uwezo watoa huduma wa vituo vya afya kuhusu utekelezaji wa huduma za lishe, hatua ambayo inalenga kuboresha huduma kwa watoto na akina mama.
Aidha, Bi Sipira alieleza kuwa wasindikaji wa unga wa mahindi wamepatiwa vifaa maalum vya kuongeza virutubishi (vinyunyizi) na mashine zao kufungiwa mifumo ya kuongeza virutubishi kwenye unga, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kupambana na upungufu wa vitamini na madini.
Kikao hicho kimeonyesha dhamira ya pamoja ya Halmashauri, viongozi na wadau katika kuhakikisha hali ya lishe inazidi kuimarika hasa kwa watoto, ili kujenga kizazi chenye afya bora na chenye mchango chanya kwa taifa.
Halmashauri ya Wilaya Songea
Anuani ya Posta: P.o.box 995, Songea
Simu: 2602320 / 2602176
Simu ya mkononi:
Barua pepe: dedsongea@songeadc.go.tz
Copyright ©2017 songeadc.go.tz. Haki imehifadhiwa