TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU mkoani Ruvuma imemfikisha katika Mahakama ya Wilaya ya Namtumbo Mkuu wa shule ya sekondari Nanungu Mohamed Shafii Ngonyani kwa makosa ya rushwa.
Akizungumza na wanahabari ofisini kwake Mahenge mjini Songea,Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Ruvuma Owen Jasson amesema Mkuu huyu wa shule na aliyekuwa Msimamizi Mkuu wa Mitihani ya kidato cha sita mwaka huu 2019 Vitus Johnson Matembo wanakabiliwa na makosa ya rushwa kinyume na kifungu cha 15 cha sheria ya kuzuia na kupambana na Rushwa Namba 11 ya mwaka 2007.
Jasson amebainisha kuwa Mei 7,2019 Ofisi ya TAKUKURU ilipokea taarifa kutoka chanzo cha siri ikimtuhumu Mkuu wa shule hiyo kwa makosa ya kuwashawishi wasimamizi wa mitihani ya kidato cha sita 2019 katika shule hiyo kwa kutaka kuwapatia fedha za hongo kiasi cha shilingi 100,000 ili walegeze masharti ya usimamizi wa mitihani kwa wanafunzi wanaofanya mitihani katika shule hiyo.
“Baada ya kupokea taarifa hiyo,uchunguzi ulifanyika ambapo ilithibitika kwamba ni kweli washitakiwa hao wawili walishirikiana kufanya kitendo cha rushwa ambapo Ndugu Vitus Johnson Matembo alishawishika na kupokea fedha hizo ili akagawane na wenzake’’,alisisitiza Jasson.
Hata hivyo Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Ruvuma amesema wenzake walikataa kushawishika na kwamba watuhumiwa hao wawili wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Namtumbo na kusomewa mashitaka yao.
Jasson kupitia kwa wanahabari amewapongeza wasimamizi wote wa mitihani ya kidato cha sita waliokataa vishawishi hivyo vya rushwa na kusimamia mitihani hiyo kwa uadilifu kama inavyotakiwa.
Halmashauri ya Wilaya Songea
Anuani ya Posta: P.o.box 995, Songea
Simu: 2602320 / 2602176
Simu ya mkononi:
Barua pepe: dedsongea@songeadc.go.tz
Copyright ©2017 songeadc.go.tz. Haki imehifadhiwa