MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas amefanya ziara ya ukaguzi wa miradi ya Boost, Swash na Lanes inayotekelezwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Songea leo Juni 27, 2023 ambapo amekagua miradi iliyopo katika Kata ya Parangu, Peramiho na Mpitimbi.
Miradi aliyoikagua ni Pamoja na mradi wa ujenzi wa vyoo matundu 15 (SWASH) unaotekelezwa kwa fedha kiasi cha shilingi milioni 37.6 kutoka Serikali Kuu, mradi wa ukarabati wa kituo cha walimu (TRC) unaotekelezwa kwa fedha kiasi cha shilingi milioni 22 na mradi wa madarasa mawili ya Awali ya mfano na matundu ya vyoo unaotekelezwa kwa fedha kiasi cha shilingi milioni 66.3
Akizungumza Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa Kanali Thomas amewataka Viongozi, wataalam na wananchi kulinda na kusimamia miradi ipasavyo kwani baadhi ya mafundi wasiposimamiwa wanafanya kazi kwa kulipua na miradi inakosa ubora hivyo wajitahidi kuisimamia ili iweze kukamilika kwa viwango na ubora unaotakiwa.
‘‘Wananchi mnao wajibu wa kusimamia kwani hii miradi ni ya kwenu hivyo hakikisheni mnaisimamia vizuri ikamilike kwa ubora ili iweze kutumika kwa vizazi na vizazi’’, amesisitiza Kanali Thomas.
Aidha, Kanali Thomas amewasisitiza mafundi kuongeza kasi ya ujenzi ili madarasa na vyoo viweze kukamilika na kutumika na wanafunzi mara shule zitakapofunguliwa na amewataka wananchi zinapohitajika nguvu zao wawajibike ipasavyo.
Akizungumza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea Ndg. Neema Maghembe kwa niaba ya uongozi wa Halmashauri ametoa shukrani kwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na Mbunge wa Jimbo la Peramiho Mhe. Jenista Joakim Mhagama kwa kuendelea kuleta fedha ambazo zinaboresha miradi ya maendeleo katika Halmashauri.
Vilevile ameishukuru ofisi ya Mkuu wa Mkoa kwa kuendelea kutembelea, kukagua na kushauri juu ya miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika Halmashauri.
Halmashauri ya Wilaya Songea
Anuani ya Posta: P.o.box 995, Songea
Simu: 2602320 / 2602176
Simu ya mkononi:
Barua pepe: dedsongea@songeadc.go.tz
Copyright ©2017 songeadc.go.tz. Haki imehifadhiwa