MKUU wa Wilaya ya Songea Mheshimiwa Pololet Kamando Mgema ameongoza hafla fupi ya utiaji saini ya Mkataba wa usimamiaji wa afua za Lishe na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea Ndugu Neema Maghembe.
Hafla hiyo imefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Mkurugenzi Lundusi-Peramiho ambayo imeudhuriwa na Watendaji Kata na baadhi ya wataalamu wa Halmashauri.
Akizungumza Mkuu wa Wilaya amesema suala la usimamiaji wa Mkataba wa Lishe limekua likifanyika kwa miaka mitano kuanzia ngazi ya Wizara, Mkoa, Wilaya, Kata hadi ngazi ya Kijiji hivyo lengo la Wilaya ni kuhakikisha inasimamia ipasavyo utekelezaji wa Afua za Lishe na kuchukua hatua madhubuti za kupunguza hali duni ya lishe.
‘’Rai yangu kwenu ni kwamba Mkataba huu utusaidie kubaini changamoto zilizopo katika maeneo yetu na kuchukua hatua madhubuti za kupunguza hali duni ya Lishe hususani udumavu wa watoto wenye umri chini ya miaka mitano ambayo ni asilimia 33 kwa mujibu wa tafiti ya Lishe Kitaifa ya Mwaka 2018’’, amesisitiza Mhe.Mgema.
Aidha amesema Halmashauri inatakiwa kufanya tathmini ya utekelezaji wa Mkataba wa Lishe mara nne kwa mwaka ili kuweza kutambua mwenendo wa utekelezaji wa afua za Lishe katika Kata na Vijiji pamoja na kutambua na kuzitatua changamoto ambazo jamii inayokutana nazo.
‘’Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan anataka kukomesha Utapiamlo na udumavu wa akili kwa watoto ambao unasababishwa na lishe duni hivyo tunatakiwa kuboresha hali ya Lishe ili kupunguza athari hizo katika Halmashauri, Kata na Mtaa’’, amesema Mhe.Pololet.
Hata hivyo amewaagiza kila Mtendaji wa Kata ahakikishe anasimamia ipasavyo utekelezaji wa Lishe kwa kutembelea katika jamii kutafuta taarifa za hali ya Lishe kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano na kufanya ufuatiliaji kwa watoto ambao wameacha matibabu ya Utapiamlo kwa kushirikiana na wataalamu wa afya pamoja na kutoa elimu ya vyakula vya Lishe.
Pia amewataka Watendaji wa Kata kutembelea katika shule za msingi na kuhakikisha kwamba wanafunzi wanapata chakula na kushirikisha wanajamii juu ya athari ambazo mwanafunzi anaweza kukutana nazo juu ya ukosefu wa Lishe.
Kwaupande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea Ndugu Neema Maghembe amesema tathmini ya Lishe ni zoezi Mtambuka linalopaswa kutekelezwa na Viongozi na wananchi wanao wahudumia.
‘’Nipende kusema kwamba yote uliyoyasema Mkuu wetu wa Wilaya tumeyapokea na tunaenda kuyafanyia kazi ili kuhakikisha zoezi hili la kusimamia Lishe na Mikataba ambayo tumesaini tunaenda kuitekeleza kama vile yalivyo makubaliano ya Serikali’’, amesema Ndugu Neema.
Nae Afisa Lishe Wilaya Joyce Kamanga amesema katika jitihada za kuhakikisha wanaondoa janga la utapiamlo wakishirikiana na Viongozi wa Kata na Kijiji watatoa mafunzo kwa jamii na kuonesha kwa vitendo uaandaaji, upishi na matumizi bora ya vyakula vya lishe kwa wanajamii.
Halmashauri ya Wilaya Songea
Anuani ya Posta: P.o.box 995, Songea
Simu: 2602320 / 2602176
Simu ya mkononi:
Barua pepe: dedsongea@songeadc.go.tz
Copyright ©2017 songeadc.go.tz. Haki imehifadhiwa