Mbunge wa Jimbo la Peramiho na Waziri wa Afya, Mheshimiwa Jenista Mhagama, ameungana na wakazi wa kijiji cha parangu kitongoji cha Magigi katika kuhamasisha zoezi la wananchi kujisajili kwa ajili ya uchaguzi ujao. Akizungumza mbele ya hadhara, Mheshimiwa Mhagama aliweka msisitizo kuhusu umuhimu wa ushiriki wa wananchi katika kuchagua viongozi watakaowawakilisha kwenye serikali za mitaa na ngazi za juu zaidi.
"Wananchi mna nafasi ya kipekee ya kushiriki katika kujenga demokrasia ya taifa letu. Katika kipindi hiki, tutakuwa na uchaguzi ambao utahakikisha sauti zenu zinafika juu," alisema Mhagama. Aliwahimiza wale ambao bado hawajajisajili kuchukua hatua mara moja, akisisitiza kuwa hatua hii ni haki yao ya kikatiba na kidemokrasia.
Wakati akitoa pongezi kwa mafanikio yaliyopatikana hadi sasa katika zoezi la usajili, Mhagama alisema kuwa zaidi ya asilimia 50 ya wananchi katika Jimbo lake tayari wamejisajili, huku baadhi ya vitongoji vikifikia asilimia 87.3 ya usajili.
"Ni muhimu sana kujiandikisha kwa ajili ya uchaguzi ili kuweza kuchagua viongozi wanaowajibika kuhakikisha maendeleo kuanzia ngazi ya kitongoji hadi taifa," alisisitiza Mhagama. Pia aliongeza kuwa serikali imeweka utaratibu bora kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa njia huru na haki.
Kwa mujibu wa taarifa za sensa ya watu na makazi, kitongoji hicho cha Magigi kina idadi ya wakazi wapatao 48 ambao wanaotakiwa kujiandikisha, ambapo tayari wakazi 44 wameshajisajili, na hivyo kuwataka wale waliobaki kujiandikisha mapema.
Pia Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Songea Thomas Masolwa, ametoa wito kwa wananchi wa Parangu na maeneo ya jirani kuendelea kumuunga mkono Mbunge wao katika safari ya kujiandikisha katika Daftari la Wapiga Kura. Akizungumza katika mkutano na wananchi, Masolwa alisisitiza umuhimu wa kujiandikisha kwa ajili ya kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uchaguzi.
"Mbunge wetu ameungana nasi kuweka sahihi yake katika daftari hili, na safari yake imekuwa na umuhimu mkubwa kwa wananchi wote wa eneo hili. Tunaendelea kushikamana na kumsaidia katika hatua hii muhimu ya kuhakikisha haki ya kupiga kura inalindwa," alisema Masolwa.
"Ni kazi yetu sote kuhakikisha tunashiriki katika mchakato huu wa kujiandikisha na tunamuunga mkono mwakilishi wetu kwa nguvu zote," aliongeza Mwenyekiti Masolwa.
Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea, Bi Elizabeth Gumbo, ambaye pia ni Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Peramiho alibainisha kuwa jumla ya vituo 453 vimeandaliwa kwa ajili ya wananchi kwenda kujisajili na baadae kupiga kura , ambapo vituo hivyo vimehakikiwa na kuwekewa mawakala wa usimamizi wa uchaguzi. Kila kituo kitakuwa na mawakala wa vyama vya siasa ili kuhakikisha uwazi na uadilifu wakati wa mchakato wa kupiga kura.
Bi Gumbo pia alisisitiza umuhimu wa mawakala kutoka vyama vyote kuhakikisha kuwa wanalinda maslahi ya wananchi kwa kuchunguza kwa makini uendeshaji wa zoezi hilo. Alisema kuwa tayari kuna mawakala wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) katika vituo hivyo, kuhakikisha kila kituo kinaongozwa kwa uwazi na haki. Aidha, aliongeza kuwa jukumu la mawakala ni kuchukua tahadhari na kuzingatia sheria ili kuepusha migogoro yoyote itakayoweza kujitokeza.
Msimamizi huyo alihitimisha kwa kusema kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Songea imejipanga kikamilifu kuhakikisha kuwa kila kituo kinasimamiwa kwa usahihi, na kwamba mawakala wamepewa maelekezo ya kina kuhusu taratibu za uchaguzi.
Halmashauri ya Wilaya Songea
Anuani ya Posta: P.o.box 995, Songea
Simu: 2602320 / 2602176
Simu ya mkononi:
Barua pepe: dedsongea@songeadc.go.tz
Copyright ©2017 songeadc.go.tz. Haki imehifadhiwa