.
Matumizi ya mfumo wa kielektroniki wa Ununuzi ya Serikali yaani national e Procuament System of Tanzania (NeST) yalioanza rasmi Oktoba 01, 2023, yameleta mapinduzi makubwa katika kuongeza uwazi na kupunguza mianya ya rushwa pamoja na kuongeza uwajibikaji katika mchakato wa manunuzi ya umma.
Akizungumza katika mahojiano maalum yaliyofanyika ofisini kwake leo Julai 21, 2025, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha ununuzi na Ugavi Ndg. Raymond Joseph alisema kuwa mfumo huo umekuwa chachu ya mabadiliko chanya tangu ulipoanza kutumika huku akieleza kuwa kila hatua ya mchakato wa manunuzi unarekodiwa na hivyo kurahisisha ufuatiliaji na ukaguzi.
“Mfumo huu umesaidia sana ukilinganisha na mfumo wa zaman, Kwanza kabisa umeongeza uwazi na uwajibikaji kwani kila hatua ya mchakato inarekodiwa, hii inarahisisha sana ufuatiliaji na ukaguzi wa manunuzi kwa sababu hakuna kitu kinachofanyika nje ya utaratibu,” alisema.
Katika hatua nyingine, alitaja baadhi ya faida za mfumo wa NeST kuwa ni pamoja na kupunguza matumizi ya karatasi ambayo yalikuwa yakigharimu sana Serikali kupitia mfumo wa awali, kupunguza shughuli zisizo na tija, imeongeza utunzaji wa mazingira kupitia kutotumia karatasi kwa wingi, kuokoa muda, pamoja na kupunguza mrundikano wa kazi kwa watumishi wa umma.
Aidha, Ndugu Raymond alieleza kuwa utekelezaji wa mfumo wa NeST katika Halmashauri ya Wilaya ya Songea umeendelea kuleta mafanikio, ikiwa ni pamoja na kuwahamasisha wazabuni wadogo kushiriki katika michakato ya zabuni kwa ujasiri na uaminifu.
“Mfumo huu umeongeza motisha kwa wazabuni wadogo kwani hakuna tena upendeleo au mfumo wa kumkumbatia mzabuni fulani. Kila kitu kinaendeshwa kwa uwazi, Tunawahimiza wazabuni wote kuomba zabuni pindi zinapotangazwa kwani kila mmoja ana nafasi sawa,” alisisitiza.
Mfumo wa NeST ni mojawapo ya jitihada za Serikali ya Tanzania kuhakikisha matumizi ya fedha za umma yanazingatia misingi ya uadilifu, uwazi na uwajibikaji kwa lengo la kuhakikisha thamani ya Fedha (value of money) na maendeleo ya wananchi kupitia manunuzi yenye tija.
Halmashauri ya Wilaya Songea
Anuani ya Posta: P.o.box 995, Songea
Simu: 2602320 / 2602176
Simu ya mkononi:
Barua pepe: dedsongea@songeadc.go.tz
Copyright ©2017 songeadc.go.tz. Haki imehifadhiwa