KATIBU tawala Wilaya ya Songea ndugu Pendo Daniel amewataka wananchi wa Songea vijijini kulinda miradi inayotekelezwa na mfuko wa maendeleo ya jamii wa TASAF.
Ameyasema hayo wakati akizungumza na wananchi wa Jimbo la Peramiho katika vijiji vya Parangu na Mdunduwalo wakati wa kikao cha uzinduzi wa miradi.
"Nitoe rai kwa viongozi mliopo hapa nanyi mna jukumu la kuhakikisha kwamba mnasimamia mradi huu kwa weledi mkubwa ili mradi ulete matunda tunayoyatarajia na mwisho kuondokana na kero ya kukosa mahitaji muhimu", amesisitiza ndugu Pendo.
Kwaupande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea Mheshimiwa Menas Komba amezitaka kamati zilizochaguliwa katika mkutano wa hadhara kuonesha uaminifu mkubwa katika kusimamia miundombinu ya ujenzi.
"Ninataka kuwasisitiza mnapokwenda kutekeleza mradi huu kila mmoja awe sehemu ya huu mradi kwa kushiriki vyema kwenye kusimamia na kulinda miundombinu na sio kuwaachia wanakamati pekee", amesisitiza Mhe.Menas.
Aidha Viongozi wote wameishukuru Serikali ya awamu ya sita chini ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na Mbunge wa Jimbo la Peramiho Mheshimiwa Jenista Joakim Mhagama kwa kuweza kuleta fedha kiasi cha zaidi ya Milioni 395 kwaajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo.
Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea ndugu Neema Maghembe ameahidi kushirikiana vyema na timu ya wataalamu, Waheshimiwa Madiwani wakiongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri Mhe.Menasi Komba, kamati zilizoundwa na wananchi kwa ujumla ili kuhakikisha mradi huu unakua wenye thamani halisi ya fedha iliyoletwa.
Akizungumza Afisa ufuatiliaji TASAF Wilaya Edwin Mlowe ambae amemwakilisha Mkurugenzi wa TASAF kutoka makao makuu amesema lengo la uzinduzi huo ni pamoja na kuzitambulisha kamati na kupeana majukumu ili kuanza kutekeleza miradi hiyo.
Amesema mradi wa TASAF umeleta fedha kiasi cha zaidi ya shilingi Milioni 225 kwa Kijiji cha Parangu sawa na asilimiili 90 kukamilisha mradi wa stendi ya mabasi, matundu ya vyoo manne na maegesho ya magari pamoja na utengenezaji wa vigae.
Pia Kijiji cha Mdunduwalo kimepokea fedha kiasi cha zaidi ya shilingi Milioni 170 sawa na asilimia 90 kukamilisha mradi wa nyumba ya mganga wa hospitali ambayo ni mbili kwa moja, mradi wa uchimbaji wa kisima cha maji pamoja na matundu ya vyoo sita.
"Hizo asilimia 10 zinazobaki wanakijiji mnawajibu wa kujitolea na kuzikamilisha kwa kushiriki shughuli mbalimbali Kama kuchimba msingi, kusogeza maji, mchanga, tofali na kushusha vifaa kutoka wenye gari hivyo nawaomba tuwape ushirikiano wa kutosha Serikali ya Kijiji na kamati iliyochaguliwa", amesisitiza Mlowe.
Wakizungumza wananchi wa Kijiji cha Parangu na Mdunduwalo wameishukuru Serikali ya awamu ya sita ikiongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Mbunge wa Jimbo la Peramiho Mheshimiwa Jenista Joakim Mhagama na Mkuu wa Wilaya Mhe.Pololet Mgema kwa kuendelea kuwakumbuka na kuwapelekea fedha za kukamilisha miradi ya maendeleo.
Pia wamewashukuru Viongozi wa Chama wakiongozwa na Mhe.Menasi Komba, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea ndugu Neema Maghembe na Viongozi wote wa ngazi ya Kata na Kijiji kwa kushirikiana nao vyema katika kuhakikisha miradi ya maendeleo inakamilika kwa wakati na viwango vinavyokubaliwa.
TASAF ni chombo cha Serikali ambacho kinasaidiana na vyombo vingine kinasaidia jitihada za kuondoa kero ya umaskini, upatikanaji wa maji safi na salama, elimu na afya ili kujenga jamii iliyo Bora.
Halmashauri ya Wilaya Songea
Anuani ya Posta: P.o.box 995, Songea
Simu: 2602320 / 2602176
Simu ya mkononi:
Barua pepe: dedsongea@songeadc.go.tz
Copyright ©2017 songeadc.go.tz. Haki imehifadhiwa