Maafisa watendaji wa kata 6 za Halmashauri ya wilaya ya Songea wamekabidhiwa pikipiki 6 zilizotolewa na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kwaajili ya watendaji kata nchini lengo likiwa ni kuboresha mazingira ya utendaji kazi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
Katika mgao wa awamu ya kwanza Pikipiki hizo zimetolewa kwa kata 6 kati ya kata 16 za Halmashauri ya Wilaya ya Songea.Mgao huo umefanyika Kwa kuzingatia Kata zilizopo pembezoni ambazo ni Mhukuru, Ndongosi, Kilagano, Matimira, Lilahi na Kizuka.
Zoezi la Kukabidhi pikipiki kwa Maafisa watendaji wa kata limefanyika katika viunga vya Halmashauri na kuudhuriwa na Mwenyekiti wa Halmashauri Mhe. Menas Komba, Waheshimiwa Madiwani wa kamati ya fedha, Mkurugenzi Mtendaji Ndugu Neema Maghembe, Wakuu wa Idara na Vitengo, Watendaji wa Kata pamoja na timu ya Wataalamu.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea Mheshimiwa Menas Komba na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea Ndg. Neema Maghembe wameongoza zoezi hilo la Kukabidhi pikipiki kwa maafisa watendaji kata.
Viongozi hao wamemshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kugawa pikipiki hizo kwa Maafisa watendaji wa kata ili kuboresha mazingira ya utendaji kazi katika utoaji wa huduma kwa wananchi. Pia Viongozi hao wamewaelekeza Maafisa hao Kutumia Pikipiki hizo kwa ajili ya kazi iliyokusudiwa na serikali ya kuwahudumia wananchi huku wakiwasisitiza kuzitunza na kuzithamini kwa kutambua kuwa ni mali ya Umma.
Aidha Maafisa watendaji kata hao wamemshukuru Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa mgao huo wa pikipiki na kuahidi kutumia pikipiki hizo kwa matumizi mazuri ya kiofisi ili kutoa huduma bora kwa wananchi ili kuleta maendeleo.
Halmashauri ya Wilaya Songea
Anuani ya Posta: P.o.box 995, Songea
Simu: 2602320 / 2602176
Simu ya mkononi:
Barua pepe: dedsongea@songeadc.go.tz
Copyright ©2017 songeadc.go.tz. Haki imehifadhiwa