Halmashauri ya wilaya ya Songea imetoa mafunzo ya mfumo wa FFARS na Planrep kwa wataalamu wake ili waweze kuitumia mifumo hiyo kwa ufanisi. Mafunzo hayo yamefanyika kuanzia tarehe18/09/2017. Mpaka tarehe 22/09/2017. Wataalamu hao kwa sasa wanamudu kuitumia mifumo hiyo kwa ufanisi mkubwa.
Akifungua mafunzo hayo Afisa Mipango wa Halmashauri ya wilaya ndugu Shaban Millao amewataka wataalam hao kutumia vizuri muda wa mafunzo ili waweze kuitumia kwa ufanisi na ilete tija kwa Halmashauri ya Wilaya ya Songea na Taifa kwa ujumla. Amesema malengo makuu ya serikali ni kuhakikisha mifumo hiyo inatumika ili kupunguza gharama zisizo za lazima katika uandaaji wa bajeti za Halmashauri na utoaji wa taarifa za kifedha kwa vituo vya kutolea huduma.
Afisa Tehama wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea ndugu John Luoga amewataka kutumia mifumo hiyo kwa uangalifu na umakini pamoja na kuzingatia taratibu kwani mifumo hiyo haifuti taratibu zinazotumika kwa sasa bali inarahisisha upatikanaji wa taarifa na kupunuza matumizi ya karatasi.
Mafunzo hayo yalitolewa na wataalamu wa ndani waliopatiwa mafunzo ya mifumo hiyo Mkoani Mtwara mwezi Julai 2017. Wataalam hao ni Afisa Mipango ndugu. Shaaban Millao, Afisa Tehama ndugu. John Luoga, Mganga mkuu wa Wilaya ndugu. Yesaya Mwasubila, Katibu wa Afya ndugu Sixmund Maseti na Mhasibu Blandina Kimaro. Mafunzo hayo yameendeshwa kwa siku tano na yametolewa kwa washiriki 184 kutoka katika Idara, vitengo na Vituo vya kutolea huduma kwa jamii.
Mfumo wa Planrep ni mfumo ulioboreshwa kutoka kutumika katika kompyuta pekee na kufikia kutumika katika mtandao wa intaneti. Mfumo huo utapunguza gharama kubwa za uandaaji wa bajeti za halmashauri na kuwezesha kutuma bajeti hizo mkoani na baadae wizarani kupitia mfumo huo.
Mfumo wa FFARS ni mfumo wa utoaji taarifa za kifedha kwa vituo vya kutolea huduma kama shule za msingi, shule za sekondari , zahanati na vituo vya Afya. Watumiaji wa mfumo huu wataweza kuandaa taarifa za kifedha watakazokuwa wanazitumia kwa shughuli mbalimbali katika vituo vyao.
Mafunzo hayo kwa wakuu wa Idara na vitengo na wasaidizi wao, wakuu wa shule, pamoja na wakuu wa vituo vya afya na zahanati yalifungwa na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ndugu Tanu Kameka.
Halmashauri ya Wilaya Songea
Anuani ya Posta: P.o.box 995, Songea
Simu: 2602320 / 2602176
Simu ya mkononi:
Barua pepe: dedsongea@songeadc.go.tz
Copyright ©2017 songeadc.go.tz. Haki imehifadhiwa