Halmashauri ya Wilaya ya Songea kupitia Kitengo cha Ustawi wa Jamii imeadhimisha Siku ya Wazee Duniani katika Kata ya Matimila, ikiwa na lengo la kuthamini na kutambua mchango mkubwa wa wazee katika ujenzi wa Taifa. Maadhimisho haya yamebeba ujumbe mzito wa kuimarisha huduma kwa wazee na kuhakikisha wanazeeka kwa heshima, sambamba na kuwapa fursa ya kupimwa afya bure, kuonesha bidhaa za kilimo, na kucheza ngoma za asili.
Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo alikuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea, Mheshimiwa Menans Komba, ambaye katika hotuba yake alitoa pongezi kubwa kwa wazee wa kata hiyo kwa mchango wao mkubwa katika kuleta maendeleo, akiwaita kuwa "hazina kubwa ya Taifa" kwani nguvu na juhudi walizoweka katika ujana wao zimechangia maendeleo tunayoyaona sasa.
“Wazee ni nguzo muhimu sana katika jamii yetu. Maendeleo yote tunayojivunia hivi sasa yamewekwa msingi na juhudi zenu. Ndio maana tunasema wazee ni dawa ni lazima tuwalinde, tuwaheshimu, na kuwashukuru kwa yote waliyotufanyia,” alisema Mheshimiwa Komba.
Akitoa wito kwa vijana, Mheshimiwa Komba aliwasihi waishi kwa amani na wazee, akieleza kuwa wazee wamepitia mengi na wanazo hekima zinazoweza kusaidia kuongoza vizazi vijavyo. “Vijana, hakikisheni mnawaheshimu na kuishi vizuri na wazee. Popote ambapo hakuna wazee, hakuna maendeleo. Sisi kama viongozi tutaendelea kuweka mazingira mazuri ya kuwaenzi wazee wetu, ili hatimaye vizazi vyetu navyo viweze kunufaika na matunzo hayo,” aliongeza.
Katibu wa Baraza la Wazee la Halmashauri ya Wilaya ya Songea, Ndugu Philip Katyale, alitoa shukrani zake kwa Mwenyekiti wa Halmashauri na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea kwa juhudi kubwa wanazozifanya chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais, hususan katika utekelezaji wa maagizo ya upimaji wa afya bure kwa wazee siku hiyo.
“Tumefanikiwa kwa kiasi kikubwa kupunguza mauaji ya wazee, jambo linaloonyesha kuwa Halmashauri yetu iko bega kwa bega na wazee katika kuhakikisha usalama wao. Maadhimisho haya na huduma ya afya bila malipo ni ushahidi wa juhudi hizo,” alisema Ndugu Katyale.
Lazarus Mapunda, mmoja wa wazee waliohudhuria maadhimisho hayo, alitoa shukrani zake kwa Mwenyekiti wa Halmashauri kwa kujitolea kwake kuhakikisha matatizo yanayowakumba wazee na jamii kwa ujumla yanapatiwa ufumbuzi haraka. “Juzi tu tulipokuwa na tatizo la kukatika kwa maji katika kata yetu, Mheshimiwa Mwenyekiti alikuwa mstari wa mbele kuhakikisha tatizo hilo linashughulikiwa na huduma ya maji inarejea mara moja,” alisema Mapunda.
Kwa mwaka huu, maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani katika Wilaya ya Songea yamefanyika yakiwa na kaulimbiu inayosema, "Tuimarishe Huduma kwa Wazee, Wazee Wazeeeke kwa Heshima". Kaulimbiu hii inalenga kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa kuwa na huduma bora kwa wazee na kuwaheshimu kama nguzo muhimu katika jamii. Mbali na upimaji wa afya bure, maadhimisho hayo yalipambwa na burudani ya ngoma za asili pamoja na maonesho ya kilimo cha uoteshaji uyoga, shughuli zilizovutia na kuleta furaha kwa wazee na wakazi wa Matimila kwa ujumla.
Kwa miaka yote, maadhimisho haya yamekuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha mahusiano kati ya wazee na vijana huku yakiwa sehemu muhimu ya kuenzi mchango wa kundi hili muhimu katika jamii.
Halmashauri ya Wilaya Songea
Anuani ya Posta: P.o.box 995, Songea
Simu: 2602320 / 2602176
Simu ya mkononi:
Barua pepe: dedsongea@songeadc.go.tz
Copyright ©2017 songeadc.go.tz. Haki imehifadhiwa