MKUU wa Wilaya ya Songea Mhe. Kapenjama Ndile amefanya ziara ya ukaguzi wa miradi ya BOOST na SWASH inayotekelezwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Songea.
Ziara hiyo imefanyika tarehe 23 Juni 2023 ambapo aliambatana na Mkurugenzi Mtendaji Ndg. Neema Maghembe Pamoja na timu ya Wataalamu.
Mhe. Ndile akiwa katika ziara hiyo amekagua ujenzi wa mradi wa BOOST wa vyumba viwili vya madarasa na matundu matatu ya vyoo katika shule ya msingi Matama ambapo mradi unatekelezwa kwa fedha kiasi cha shilingi Milioni 53.1 kutoka Serikali kuu.
Pia Mhe. Ndile amekagua ujenzi wa mradi wa uboreshaji wa miundombinu ya shule za masingi na Awali (BOOST) wa vyumba viwili vya madarasa na matundu matatu ya vyoo katika shule ya msingi Nakawale unaotekelezwa kwa fedha kiasi cha shilingi Milioni 53.1 kutoka Serikali Kuu.
Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya amekagua ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa ya Awali ya mfano na matundu ya vyoo katika shule ya msingi Humbaro unaotekelezwa kwa fedha kiasi cha shilingi Milioni 66.3.
Vilevile amekagua ujenzi wa mradi wa SWASH wa ujenzi wa vyoo matundu 13 katika shule ya msingi Lihuhu unaogharimu fedha kiasi cha shilingi Milioni 33,743,862 pia ujenzi vyoo matundu 14 katika shule ya msingi Lung‘oo unaogharimu fedha kiasi cha shilingi milioni 36,193,862.
Mradi mwingine uliokaguliwa ni Pamoja na mradi wa ujenzi wa vyumba tisa vya madarasa, mabweni manne na vyoo matundu 14 katika shule ya sekondari Mpitimbi ambao unatekelezwa kwa fedha kiasi cha shilingi Milioni 751.8 kutoka Serikali kuu ambao una lengo la kuongeza miundombinu ya wanafunzi wa kidato cha tano.
Akizungumza katika ukaguzi wa miradi hiyo amesisitiza miradi ikamilike ndani ya muda uliopangwa na kwa viwango na ubora unaokubalika na Serikali.
‘‘Viongozi wote mnaohusika na miradi hii jitahidini kutoa hamasa kwa wananchi pale ambapo nguvu za wananchi zinahitajika waweze kushiriki kikamilifu miradi iweze kukamilika kwa wakati’’, amesisitiza Mhe. Ndile.
Akihitimisha ziara hiyo Mkuu wa Wilaya amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuleta fedha hizo za kuboresha miundombinu ya Elimu, pia ametoa rai kwa walimu wa shule kuhakikisha wanafanya jitihada za kupandisha ufaulu kwa wanafunzi kama shukrani kwa Mheshimiwa Rais.
Halmashauri ya Wilaya Songea
Anuani ya Posta: P.o.box 995, Songea
Simu: 2602320 / 2602176
Simu ya mkononi:
Barua pepe: dedsongea@songeadc.go.tz
Copyright ©2017 songeadc.go.tz. Haki imehifadhiwa