Mbunge wa Jimbo la Peramiho na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mheshimiwa Jenista Joakim Mhagama ametembelea na kuweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa tanki la kuhifadhia maji katika Kijiji cha Peramiho A.
Akizungumza Mheshimiwa Jenista amewasisitiza wananchi kutunza na kulinda miundombinu ya mradi huo wa maji ili uendelee kuwanufaisha.
“Kukamilika kwa mradi huu ambao umefikia asilimia 98 utasaidia kwa kiasi kikubwa kuondoa tatizo la uhaba wa maji ambalo limekuwa likiwasumbua kwa mda mrefu hivyo tuna kila sababu ya kumshukuru Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutuletea fedha hizo”, amesisitiza Mheshimiwa Jenista.
Akisoma taarifa Mhandisi wa maji Wilaya Triphon Mwanangwa amesema mradi hadi kukamilika utagharimu fedha kiasi cha shilingi milioni 285 kutoka Serikali Kuu.
“Lengo la mradi ni kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi wa vijiji vya Peramiho A na Nguvu moja ambao walikuwa wanapata maji kwa mgawo kwa kuwa tanki lililokuwa linatumika lilikuwa ni dogo (lita 65,000) tu ukilinganisha na mahitaji ya maji kwa wananchi”, amesema Mhandisi Mwanangwa.
Aidha, Mhandisi ameongeza kuwa mradi huu unatekelezwa kwa fedha za P for R (Payment for Result) yaani Lipa kwa matokeo ambapo kukamilika kwa ujenzi huu watu wapatao 6,267 watanufaika na huduma ya maji.
Chanzo cha maji ni chemichemi za asili chenye uwezo wa kuzalisha lita 133,000 kwa siku na uwezo wa pampu ni lita 17,000 kwa saa.
Wakizungumza wananchi wa Kata ya Peramiho wamemshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuleta fedha za kutekeleza mradi huo wa maji.
Halmashauri ya Wilaya Songea
Anuani ya Posta: P.o.box 995, Songea
Simu: 2602320 / 2602176
Simu ya mkononi:
Barua pepe: dedsongea@songeadc.go.tz
Copyright ©2017 songeadc.go.tz. Haki imehifadhiwa