Wanafunzi wa kidato cha Sita katika shule ya sekondari Maposeni wilayani Songea mkoani Ruvuma wanaorejea shuleni,wamewatoa hofu wazazi na walezi wao kwamba wapo salama dhidi ya maambukizi ya homa kali ya Mapafu (Covid 19).
Wakizungumza kwa niaba ya Wanafunzi wenzao Anastazia Christopher na Isaya Mlelwa wamesema wapo salama kwasababu walimu wanachukua tahadhali zote za kujikinga na virusi vya corona na kwamba wanafunzi wote wanaoripoti shuleni hapo,wana vifaa muhimu vikiwemo vitakasa mikono na uvaaji wa barakoa kwa kila mwanafunzi.
Mkuu wa sekondari hiyo Dismasi Nchimbi amezitaja tahadhari nyingine zilizochukuliwa na shule hiyo ni kuzingatia ukaaji wa wanafunzi madarasani kwa kila darasa kukaa wanafunzi wasiozidi 20,idadi ya kulala kwenye mabweni kwa kila chumba kutoka wanafunzi wanne mpaka wawili na kila kitanda kulala mwanafunzi mmoja badala ya wawili.
Nchimbi amesema hadi kufikia Juni 3,jumla ya wanafunzi wa kidato cha sita 185 kati yao wavulana 95 na wasichana 90 wameripoti kati ya wanafunzi 222 waliosajiriwa.
Akizungumza na wanafunzi wa kidato cha sita katika sekondari ya Kigonsera kwa niaba ya wanafunzi wa kidato cha sita katika Mkoa wa Ruvuma,Mndeme amewaasa wanafunzi hao kuchukua tahadhari dhidi ya virusi vya corona kwa kuzingatia tahadhari zote zinazotolewa na Wizara ya afya.
Hata hivyo Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme amewataka wenye Mabasi ya abiria kuwa wazalendo kuwapa kipaumbele wanafunzi wanaosafiri kuelekea shuleni na vyuoni baada ya shule na vyuo kufunguliwa Juni Mosi mwaka huu.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alitangaza kufunga shule na vyuo nchini tangu Machi 17 mwaka huu kufuatia tishio la ugonjwa wa Covid 19 ambalo ni janga la dunia.
Imeandikwa na Jacquelen clavery
Afisa Habari Halmashauri ya Wilaya ya Songea
Juni 3,2020
Halmashauri ya Wilaya Songea
Anuani ya Posta: P.o.box 995, Songea
Simu: 2602320 / 2602176
Simu ya mkononi:
Barua pepe: dedsongea@songeadc.go.tz
Copyright ©2017 songeadc.go.tz. Haki imehifadhiwa