MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme amefanya ufunguzi wa maonesho ya nanenane ngazi ya Mkoa kwa kueleza mafanikio makubwa ambayo yamepatikana ikiwemo uzalishaji wa chakula cha kutosha hali ambayo imefanya Mkoa kuwa na ziada ya chakula tani 877,000.
Katika hotuba ya Mndeme ambayo ilisomwa na Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Cosmas Nsenye kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma,amesema kutokana na kuongezeka kwa uzalishaji wa mazao ya chakula Mkoa umepangiwa na serikali kununua zao la mahindi kiasi cha tani 70,000 kwa shilingi 550 kwa kilo kupitia Wakala wa Usalama wa Chakula wa Taifa(NFRA).
Hata hivyo Mndeme amesema Mkoa unatambua changamoto ya soko kwenye zao la mahindi na unaendelea na jitihada za kuwatafutia wawekezaji watakaosaidia katika usindikaji na kuongeza upatikanaji wa soko.
“Mkoa wa Ruvuma kwa mwaka 2015 ulikuwa na jumla ya ng’ombe 117,374,mbuzi 227,186,nguruwe 223,976,ambapo mwaka 2020 mifugo imeongezeka na kufanya Mkoa kuwa na ng’ombe 190,514,mbuzi 272,147,kondoo 30,625 na nguruwe 315,923’’,alisema Mndeme.
Amesema ongezeko la mifugo limesababisha kuongezeka kwa mazao ya mifugo na kufikia tani 7,851.58 za nyama ya ng’ombe,tani 4,906.65 za nyama ya mbuzi,tani 871.2 za nyama ya kondoo,tani 14,033.32 za nyama ya nguruwe na tani 179,345.
Mkuu wa Mkoa amemshukuru Rais Dkt.John Magufuli kwa kutoa kiasi cha shilingi bilioni tatu kwa ajili ya ujenzi wa machinjio ya kisasa iliyopo Manispaa ya Songea yenye uwezo wa kuchinja ng’ombe 100 na mbuzi 200 kwa siku ambapo amesema hiyo ni fursa kwa wafugaji.
Halmashauri ya Wilaya Songea
Anuani ya Posta: P.o.box 995, Songea
Simu: 2602320 / 2602176
Simu ya mkononi:
Barua pepe: dedsongea@songeadc.go.tz
Copyright ©2017 songeadc.go.tz. Haki imehifadhiwa