MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea Ndugu Neema Maghembe ambae amewakilishwa na Afisa Mipango Bw. Athuman Nyange amefungua semina ya mafunzo ya mradi wa Upandaji miti na Utunzaji wa Mazingira Songea Vijijini.
Mafunzo hayo yalifanyika katika ukumbi wa CCM Wilaya na kuudhuriwa na wajumbe mbalimbali wakiwemo Walimu wa mazingira wa shule za msingi na wawakilishi yaani Mabalozi wasimamizi wa mazingira ngazi ya Kata na Vijiji.
Mafunzo hayo yaliratibiwa na Taasisi isiyokuwa ya Kiserikali inayoitwa Muunganisho wa Ujasiriamali Mijini na Vijijini (MUMIVI) ambayo inajishughulisha na Upandaji miti Pamoja na Utunzaji wa mazingira katika ngazi ya jamii.
Akizungumza Kaimu Mkurugenzi katika mafunzo hayo amewahasa wajumbe waliodhuria mafunzo hayo Kwenda kutoa elimu kwa jamii juu ya upandaji miti na utunzaji wa mazingira kwani kiwango cha uharibifu wa mazingira kipo juu sana hivyo elimu itolewe mapema.
“Elimu mtakayoipata hapa ikawe chachu na muwe mabalozi wazuri kwa Kwenda kuwaelimisha wananchi juu ya upandaji miti na utunzaji wa mazingira”, amesisitiza Bw. Nyange.
Akizungumza Mkurugenzi wa Taasisi hiyo Koyigila Kazuzi amesema lengo la Taasisi ya MUMIVI ni kuunganisha watumiaji wa kuni na mkaa kuwa na wajibu wa kurejesha miti iliyopotea na inayoendelea kupotea kwa kutoa elimu na mafunzo juu ya upandaji miti na kuitunza, hivyo katika Halmashauri ya Wilaya ya Songea wamedhamiria kuanzisha miradi hiyo kwa kupanda miche ya miti katika shule za msingi mbili katika kila Kata.
Ameongeza kuwa kama jamii itazingatia utunzaji wa mazingira kwa kupanda miti na kuitunza hivyo watakuwa wametunza vyanzo vya maji na kuboresha mazingira kwa kiasi kikubwa hivyo vizazi vijavyo vitanufaika na uhifadhi huo.
Nae Afisa Misitu Wilaya ya Songea Zakayo Kaunda amesema Agizo la Serikali ni kila Halmashauri ihakikishe inapanda jumla ya miti Milioni 1,500,000 kwa mwaka hivyo Halmashauri ya Wilaya ya Songea imefanikiwa kupanda miti Milioni 1,200,000 hadi sasa katika maeneo ya shule, hospitali na taasisi mbalimbali za Serikali.
Hata hivyo nae ameunga mkono jitihada za taasisi ya MUMIVI kwa kutoa mafunzo na elimu juu ya Upandaji miti na Utunzaji wa mazingira.
Pia Afisa Elimu maalumu Mwl. Sothery Nchimbi ambae pia ni mdau wa mazingira amewasisitiza walimu na wadau wote wa mazingira walioshiriki mafunzo hayo nao waende kutoa elimu hiyo kwa wanafunzi na jamii kwa ujumla hili mafunzo hayo yaweze kuleta tija.
Halmashauri ya Wilaya Songea
Anuani ya Posta: P.o.box 995, Songea
Simu: 2602320 / 2602176
Simu ya mkononi:
Barua pepe: dedsongea@songeadc.go.tz
Copyright ©2017 songeadc.go.tz. Haki imehifadhiwa