Mkuu wa kitengo cha huduma za sheria Halmashauri ya Wilaya ya Songea Wakili msomi Pascal Kapinga ameongoza ziara ya kutoa mafunzo kwa wajumbe wa Mabaraza ya Kata ya Muhukuru Barabarani na Muhukuru Lilahi, akisisitiza umuhimu wa usuluhishi katika kutatua migogoro ya ardhi kwa njia ya haki na uadilifu.
Katika ziara hiyo, Wakili. Kapinga alikazia wajumbe wa Mabaraza hayo kutenda haki bila kuingiliwa na maslahi binafsi, huku akieleza kuwa jukumu la Mabaraza hayo ni kusuluhisha migogoro na si kutoa hukumu. Alisema, "Zingatieni uadilifu wa kazi yenu, kazi yenu sio ndogo ni kazi kubwa lakini niwaombe msitoe hukumu katika migogoro Bali ni usuluhishi tu; Shauri likishindikana kwenye baraza, wadaawa wapewe hati ya usuluhishi ili kwenda hatua nyingine za kisheria kutafuta haki
Hatua hii ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Tanzania kuboresha utatuzi wa migogoro ya ardhi kupitia Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, kwa kuanzisha mwongozo wa usuluhishi wa migogoro ya ardhi katika Mabaraza ya Kata. Mwongozo huo unalenga kuweka utaratibu rahisi, wa haki na wa maridhiano katika jamii, ili kumaliza migogoro kwa njia ya usuluhishi badala ya kufika moja kwa moja katika mfumo wa mahakama.
Mafunzo hayo yanatarajiwa kuwa na manufaa kwa wajumbe wa Mabaraza ya Kata katika kutatua migogoro ya ardhi kwa njia ya usuluhishi, ambayo inajulikana kwa urahisi, haraka, na gharama nafuu kwa wananchi. Aidha, Wakili. Kapinga alisisitiza kuwa ni muhimu kwa wajumbe wa Mabaraza ya Kata kuepuka vitendo vya rushwa kwani utendaji wa haki unahitaji kuwa wa wazi na waaminifu kwa pande zote.
Wajumbe wa Mabaraza ya Kata walimshukuru Wakili. Kapinga kwa mafunzo hayo, wakisema kuwa walikuwa wakifanya baadhi ya maamuzi kinyume na miongozo ya utatuzi wa migogoro kwani mambo mengine walikuwa hawayafahamu. Waliahidi kuwa sasa watazingatia mafunzo na miongozo hiyo katika kutenda haki kwa manufaa ya jamii.
Halmashauri ya wilaya ya Songea kupitia kitengo cha Huduma za Sheria inaendelea kuhimiza na kuimarisha mifumo ya usuluhishi wa migogoro ya ardhi, kuhakikisha kuwa wananchi wanapata haki kwa njia rahisi, haraka na kwa gharama nafuu.
Halmashauri ya Wilaya Songea
Anuani ya Posta: P.o.box 995, Songea
Simu: 2602320 / 2602176
Simu ya mkononi:
Barua pepe: dedsongea@songeadc.go.tz
Copyright ©2017 songeadc.go.tz. Haki imehifadhiwa