HALMASHAURI ya Wilaya ya Songea imedhamiria kuandaa mipango shirikishi itakayotumiwa na Wawekezaji, Serikali ya kijiji na Halmashauri katika sekta ya Kilimo na Madini hususani makaa ya mawe.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea Mhe.Menas Komba katika kikao kilichofanyika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri Lundusi-Peramiho wakati akizungumza na kujenga uelewa kwa Wawekezaji juu ya uwajibikaji wa kampuni kwa jamii (CSR).
Amesema lengo la kuandaa mpango huu ni kuondoa migogoro isiyokuwa ya lazima na manung’uniko kati ya wawekezaji, Serikali ya kijiji na Halmashauri ya Wilaya.
‘’Nichukue nafasi hii kuwashukuru wawekezaji sisi kama Halmashauri tutafanya kazi na nyinyi kwa asilimia 100 hivyo basi tutaomba ushirikiano wenu na yale tunayokubaliana nayo yafuatwe’’, amesisitiza Mhe.Menas.
Kwaupande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea Ndugu Neema Maghembe amewataka wawekezaji kuwa wawazi na waweze kushirikisha wanajamii juu ya mradi wanaoutekeleza hii itaongeza thamani ya wawekezaji kwenye jamii.
‘’Naomba kuwashauri wawekezaji wetu kuwa wawazi kama mnatoa Shilingi Milioni sita kwa kwaajili ya kutekeleza mradi basi yote itumike kwenye mradi kwa uaminifu na muweze kushirikisha wanajamii katika ununuzi wa vifaa, pia katika kuihudumia jamii kwa asilimia 0.07 muweze kusema ni Shilingi ngapi kutoka kwenye jumla ya mauzo yenu’’, amesisitiza Ndugu Neema.
Akisoma taarifa Afisa Mazingira Makisio Chengula amesema kampuni ambazo zimekusudiwa katika mpango huu zipo sita ambazo ni Rutanza Coal Limited, AVIV Tanzania Limited, Agnes and Michael, Synergy Tanzania Company Limited, Com Coal Limited na Tuteikwa Investmant Company Limited.
Amesema mpango huu utazisaidia Serikali za vijiji kutambua miradi inayotekelezwa kwenye kata na vijiji vyao kupitia mwekezaji na itasaidia kijiji kuwa na mpango na kampuni husika.
Wakizungumza wawekezaji wameunga mkono mikakati iliyowekwa na Halmashauri, pia wamekubali kukaa pamoja na Halmashauri na kuweka mikakati juu ya kutekeleza uwajibikaji wao kwa jamii.
Halmashauri ya Wilaya Songea
Anuani ya Posta: P.o.box 995, Songea
Simu: 2602320 / 2602176
Simu ya mkononi:
Barua pepe: dedsongea@songeadc.go.tz
Copyright ©2017 songeadc.go.tz. Haki imehifadhiwa