Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo amefanya ziara ya kihistoria katika Jimbo la Peramiho, Mkoa wa Ruvuma, ambako alipokelewa kwa shangwe na maelfu ya wananchi waliofurika katika viwanja vya Abasia ya Peramiho.
Ziara hii ni sehemu ya mikakati ya Rais Samia ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo, kusikiliza kero za wananchi, na kutoa maelekezo kwa viongozi wa mikoa na wilaya.
Katika hotuba yake, Rais Samia alisifu mchango wa Kanisa Katoliki nchini, hususan katika utoaji wa huduma za kijamii kama vile elimu, afya, na maji, ambazo zimekuwa kichocheo kikubwa cha maendeleo ya jamii kwa ujumla. Alilitaja eneo la Kanisa la Peramiho kama la kihistoria, na alionyesha furaha yake kufika hapo.
Rais aliwakumbusha wananchi umuhimu wa kushiriki kikamilifu katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika tarehe 27 Novemba mwaka huu. Alisisitiza, "Mawaziri wamezungumza sana kuhusu uchaguzi mkuu, lakini mimi natumia fursa hii kuwakumbusha kuhusu uchaguzi wa serikali za mitaa. Lazima tufanye vizuri, wote wenye sifa za kugombea na kupiga kura wajitokeze kwa wingi," alisema Rais Samia huku akihimiza ushiriki wa wananchi.
Aidha, Rais Samia alitoa wito kwa wananchi wa Peramiho kuendelea kudumisha amani, upendo, na utulivu, akieleza kuwa "ama ni msingi wa maendeleo ya nchi yetu."
Mbunge wa Jimbo la Peramiho ambaye pia ni Waziri wa Afya, Mhe. Jenista Mhagama, alimshukuru Rais kwa ziara yake na mchango mkubwa wa maendeleo katika jimbo hilo. Alieleza kuwa tangu Rais Samia aingie madarakani, Jimbo la Peramiho limepata zaidi ya Shilingi Bilioni 49 kwa ajili ya miradi mbalimbali ya afya, elimu, barabara, na maji. "Tunakushukuru sana, Mhe. Rais, kwa kutuletea maendeleo makubwa katika jimbo letu," alisema Mhe. Jenista.
Katika ziara hiyo, Rais Samia alisema serikali itaendelea kuwekeza katika miradi ya maendeleo ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za kijamii kwa wakati. Ziara hiyo imeacha alama kubwa ya matumaini kwa wananchi wa Peramiho, wakitarajia maendeleo zaidi.
Halmashauri ya Wilaya Songea
Anuani ya Posta: P.o.box 995, Songea
Simu: 2602320 / 2602176
Simu ya mkononi:
Barua pepe: dedsongea@songeadc.go.tz
Copyright ©2017 songeadc.go.tz. Haki imehifadhiwa