Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea, ambaye pia ni Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Peramiho, Bi Elizabeth Gumbo, amefanya kikao na wadau wa vyama vya siasa kutoka Halmashauri hiyo, kwa lengo la kujadili maandalizi ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Katika kikao hicho, Bi Gumbo aliwataka viongozi wa vyama hivyo kuwa watulivu kuelekea uchaguzi huo, ili kuhakikisha unafanyika kwa haki, amani, na utulivu.
Akiwaeleza wajumbe wa kikao hicho, Bi Gumbo alifafanua kuwa idadi ya vitongoji katika wilaya hiyo itabaki ileile, ambayo ni 443, huku mabadiliko pekee yakiwa ni ongezeko la vituo vya kujiandikisha na kupigia kura, ambavyo sasa vimefikia 453. Alisema lengo la kuongeza vituo hivyo ni kurahisisha huduma kwa wananchi, ili wasilazimike kutembea umbali mrefu, akisisitiza kuwa vituo hivyo havina sifa ya kuwa vitongoji kwa kuwa vigezo maalum vya uanzishaji wa kitongoji havijatimia.
Aidha, Bi Gumbo aliwasihi wajumbe wa kikao hicho kutumia nafasi zao kuhamasisha wananchi kujiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura. “Zimebaki siku mbili tu za kujiandikisha. Nyinyi ndio wenye dhamana ya kuhamasisha watu wenu waliopo chini. Niwaombe sana, kwa muda huu uliobaki, mkawe mabalozi wa kuwahimiza wananchi kujiandikisha ili waweze kupata haki yao ya kikatiba ya kumchagua kiongozi anayewafaa,” alieleza Bi Gumbo.
Bi Gumbo alibainisha kuwa kwa mujibu wa kanuni na taratibu zilizopo, uongozi wa sasa utamalizika rasmi kesho, Oktoba 19, 2024. “Ni nafasi yenu sasa kuwaandaa wagombea kutoka kwenye vyama vyenu, kwani viongozi waliopo madarakani watamaliza muda wao rasmi kesho. Zoezi la uchukuaji wa fomu za kugombea nafasi mbalimbali litaanza rasmi Oktoba 26 hadi Novemba 1, 2024. Ni muhimu kufahamu kuwa fomu hizo zitatolewa tu kwa watu wenye barua ya utambulisho kutoka kwenye vyama husika,” alisisitiza.
Kwa upande wao, wajumbe wa kikao hicho walimshukuru Mkurugenzi kwa ushirikiano aliowaonyesha, huku wakimwomba aendelee kusimamia kwa umakini zoezi hilo ili uchaguzi ufanyike kwa amani, utulivu, na haki kwa kila mwanachama. Waliahidi kuwa watatekeleza wajibu wao wa kuhamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika mchakato mzima wa uchaguzi.
Halmashauri ya Wilaya Songea
Anuani ya Posta: P.o.box 995, Songea
Simu: 2602320 / 2602176
Simu ya mkononi:
Barua pepe: dedsongea@songeadc.go.tz
Copyright ©2017 songeadc.go.tz. Haki imehifadhiwa