Kaya masikini katika Halmashauri ya Wilaya ya Songea Mkoani Ruvuma zimeibua miradi 44 ya kutoa ajira za muda mfupi ambayo utekelezaji wake unatakiwa kuanza kutekelezwa mwezi Julai hadi Disemba 2021.
Mratibu wa TASAF wa Wilaya hiyo Hossana Ngunge amesema miradi iliyoibuliwa na kaya hizo ni ile ambayo haipo katika mfumo rasmi wa Serikali kama vile Wakala wa barabara za Mijini na Vijiji (TARURA) Wakala wa Maji safi na Usafi wa Mazingira pamoja na Idara ya Kilimo.
“Wataalam wanaohusika na miradi ambayo kaya hizo zimeibua watahusika kusimamia kazi hizo kwakushirikiana kwa pamoja na walengwa wenyewe na mtoa huduma wa Kijiji ambaye amepitia mafunzo ya kuhakikisha miradi inakamilika kwa viwango vinavyotakiwa”, amesisitiza Ngunge.
Ngunge ameitaja miradi hiyo kuwa ni uboreshaji wa visima vya asili,ujenzi wa barabara ujenzi wa vivuko na kilimo cha zao la korosho ambao utekelezaji wake ni matokeo ya TASAF awamu ya pili kipindi cha tatu kipindi kinachotakiwa kuanza kutekelezwa kuanzia mwezi Julai 2021.
Ameelezea masharti ya utekelezaji wa miradi hiyo kuwa miradi yote inatakiwa kutekelezwa kwa kipindi kisichozidi miezi sita na mlengwa atalipwa ruzuku ya shilingi 3000 kwa siku pia hatatakiwa kufanyakazi zaidi ya masaa 4 na kutembea umbali wa zaidi ya saa moja kufika eneo la mradi ulipo.
Amesema miradi hiyo inatekelezwa katika vijiji 32 kati ya vijiji 56 vya Halmashauri ya Wilaya ya Songea Mkoani Ruvuma na utaratibu wa kutoa ajira za muda mfupi upo tangu kipindi cha kwanza awamu ya tatu.
Baadhi ya wanakaya wanaohudumiwa na Mfuko huo wametoa wito kwa Serika kuwapa matibabu mara wanapo kwenda kwenye vituo vya kutolea huduma za Afya kwasababu hawapati huduma ya dawa kulingana na mahitaji yao.
Imeandikwa na
Jacquelen Clavery
Kaimu Afisa Habari – Songea DC.
Halmashauri ya Wilaya Songea
Anuani ya Posta: P.o.box 995, Songea
Simu: 2602320 / 2602176
Simu ya mkononi:
Barua pepe: dedsongea@songeadc.go.tz
Copyright ©2017 songeadc.go.tz. Haki imehifadhiwa