Baraza la Madiwani Halmashauri ya Wilaya ya Songea, limekaa jana, ambapo pamoja na mambo mengine, wamepitisha mikakati ya kuboresha ukusanyaji wa mapato ya Halmashauri, ambapo kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango imejipanga kuimarisha mfumo wa ukusanyaji wa ushuru na kuhakikisha mazingira bora kwa wakusanyaji
Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Songea limefanyika katika ukumbi wa Halmashauri hiyo, likiongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri, Mhe. Menans Komba, huku likihudhuriwa na madiwani kutoka kata zote 16 za Halmashauri ya Wilaya ya Songea.
.
Kikao hicho pia kilipitisha taarifa mbalimbali kutoka kamati za kudumu za halmashauri, ambazo ni Kamati ya Elimu, Afya na Maji; Kamati ya Kudhibiti UKIMWI; Kamati ya Nidhamu na Maadili; Kamati ya Uchumi, Ujenzi na Mazingira; na Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango. Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango ilionekana kuvutia zaidi hisia za wajumbe wa Baraza kwa kujadili mbinu mpya za kuongeza mapato ya Halmashauri, ikiwa ni pamoja na kuboresha vituo vya ukaguzi (mageti) ili kuhakikisha ukusanyaji wa mapato unafanyika kwa ufanisi mkubwa.
ukaguzi (mageti) ili kuhakikisha ukusanyaji wa mapato unafanyika kwa ufanisi mkubwa.
Mwenyekiti wa Halmashauri, Mhe. Menans Komba, alieleza kuwa halmashauri imeanza mchakato wa kuboresha vituo hivyo kwa kujenga mageti imara badala ya yale ya awali ya muda. "Tumeamua kujenga mageti thabiti ambayo yatawawezesha wakusanyaji wa ushuru kufanya kazi zao katika mazingira salama, hata wakati wa mvua au upepo. Kwa maeneo ambayo hayajafikiwa na huduma ya umeme, tumeweka mpango wa kutumia nishati ya sola ili wakusanyaji waweze kuchaji mashine za POS na kuendelea na kazi zao bila kikwazo," alieleza Mhe. Komba.
Aidha, alitoa shukrani kwa madiwani kwa kuwa na uzalendo wa hali ya juu katika kusimamia ukusanyaji wa mapato ndani ya kata zao. Alibainisha kuwa madiwani wamekuwa mstari wa mbele kuripoti udanganyifu unaoweza kuhujumu mapato ya Halmashauri.
"Napenda kuwashukuru kwa namna ambavyo mmekuwa makini katika kata zenu. Mmeonyesha uzalendo mkubwa kwa kutoa taarifa pale mnapohisi kuna udanganyifu katika ukusanyaji wa mapato. Hii ni hatua kubwa sana katika kuimarisha maendeleo ya Halmashauri yetu. Tutaendelea kufanya kazi kwa kushirikiana kama timu moja kwa ajili ya maendeleo," aliongeza Mhe. Komba.
Kikao hicho kilimalizika kwa madiwani kuazimia kushirikiana na kamati za Halmashauri katika kufanikisha malengo ya kuongeza mapato, huku viongozi wa Halmashauri wakiweka msisitizo katika kuimarisha uwazi na uwajibikaji kwa maendeleo endelevu.
Halmashauri ya Wilaya Songea
Anuani ya Posta: P.o.box 995, Songea
Simu: 2602320 / 2602176
Simu ya mkononi:
Barua pepe: dedsongea@songeadc.go.tz
Copyright ©2017 songeadc.go.tz. Haki imehifadhiwa