Mhe. Kapinga Aongoza Baraza la Madiwani na Kupitisha Taarifa ya Hesabu za Halmashauri ya Wilaya ya Songea kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
Kaimu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea, Mhe Simon Kapinga, ameongoza kikao muhimu cha Baraza la Madiwani kilichofanyika leo, tarehe 30 Agosti 2024, katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea. Kikao hiki kilihudhuriwa na Madiwani pamoja na wataalamu mbalimbali wa Halmashauri. Lengo kuu la kikao hicho lilikuwa ni kupokea na kupitisha taarifa ya hesabu za Halmashauri kwa mwaka wa fedha 2023/2024.
Kwa mujibu wa Sheria za Serikali za Mitaa ya mwaka 1982, kifungu namba 4, kama ilivyorekebishwa mwaka 2000, Halmashauri zote nchini zinatakiwa kufunga hesabu na kuziwasilisha kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kabla ya tarehe 31 Agosti ya kila mwaka. Mabadiliko haya yametokana na marekebisho ya waraka wa Hazina uliotolewa ili kuhakikisha kuwa hesabu za mwaka wa fedha zinakamilika na kuwasilishwa mapema, tofauti na utaratibu wa awali wa kuwasilisha hesabu hizo kabla ya tarehe 30 Septemba ya kila mwaka. Waraka huu mpya unalenga kuboresha uwazi na uwajibikaji wa fedha za umma.
Taarifa ya hesabu iliyopitishwa na Baraza la Madiwani imeonyesha mtiririko mzuri wa mapato na matumizi ya halmashauri. Kulingana na taarifa hiyo, Halmashauri ilianza mwaka wa fedha ulioishia tarehe 30 Juni 2024 ikiwa na salio la TSh 2,594,074,952.00. Jumla ya mapato kwa mwaka huo wa fedha pamoja na salio la awali yalifikia TSh 36,786,049,740.00, huku matumizi yote kwa mwaka huo yakiwa ni TSh 31,532,325,901.00. Hivyo, salio/bakaa lililokuwepo benki kufikia tarehe 30 Juni 2024 lilikuwa TSh 5,253,723,839.00.
Akizungumza baada ya kupitishwa kwa taarifa hiyo, Mhe. Kapinga aliwapongeza Madiwani kwa kazi nzuri ya kusimamia mapato na matumizi ya Halmashauri. Aidha, aliwataka kuendelea kuwa mabalozi wazuri katika kata zao, hususan wakati huu ambapo nchi inajiandaa kwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Alisisitiza umuhimu wa kuwahamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura.
“Filimbi imepigwa kutuamsha sasa, kwamba wakati umefika,” alisema Mhe. Kapinga. “Ni jukumu letu kama viongozi kuhakikisha tunawatia moyo wananchi wetu ili wajitokeze kwa wingi kujiandikisha na hatimaye kupiga kura kwa amani. Hii itasaidia kuchagua viongozi bora watakaoweza kutumikia wananchi kwa ufanisi na kuleta maendeleo ya kweli katika jamii zetu.”
Kikao hicho pia kilijadili masuala mbalimbali ya maendeleo ya Halmashauri, ikiwa ni pamoja na ukusanyaji wa mapato ya ndani, na mikakati ya kuboresha huduma kwa wananchi. Madiwani walisisitiza umuhimu wa kuendelea kushirikiana kwa karibu ili kuhakikisha kuwa Halmashauri inaendelea kusonga mbele na kufikia malengo yake ya maendeleo.
Halmashauri ya Wilaya Songea
Anuani ya Posta: P.o.box 995, Songea
Simu: 2602320 / 2602176
Simu ya mkononi:
Barua pepe: dedsongea@songeadc.go.tz
Copyright ©2017 songeadc.go.tz. Haki imehifadhiwa