Afisa Lishe wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea, Bi Joyce Sipira, akisisitiza umuhimu wa ulaji wa mazao lishe kwa wanafunzi kama njia ya kuboresha afya, kuongeza umakini darasani, na kuimarisha ufaulu wa kitaaluma.
Akizungumza leo katika mkutano na waandishi wa habari Bi Joyce alisema kuwa kampeni hiyo inalenga kuhamasisha shule za sekondari kuanza kutumia mazao lishe yaliyothibitishwa kuwa na virutubishi muhimu kwa afya ya mwanafunzi. Alieleza kuwa tayari Halmashauri kwa kushirikiana na mdau wa lishe, HarvestPlus, imeanza utekelezaji wa mpango huo katika shule mbili za sekondari: Maposeni na Magagula.
“Tulipokea maelekezo kutoka kwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ambayo nayo ilipokea ugeni kutoka kwa mdau HarvestPlus wasambazaji waliothibitishwa wa mazao lishe. Kwa kuanzia, shule mbili zimechaguliwa kama sehemu ya majaribio ya mpango huu,” alisema Bi Joyce.
Aliendelea kufafanua kuwa lengo kuu la mpango huo ni kuhakikisha kuwa wanafunzi wanapata chakula chenye virutubishi vya kutosha ili waweze kuwa makini zaidi darasani, kupunguza utoro, kuongeza ushiriki wa darasani, na kuimarisha afya kwa ujumla.
Katika mkutano huo, Bi Joyce alitaja baadhi ya mazao lishe yanayopendekezwa kuwa ni mahindi ya njano lishe, viazi vitamu vya chungwa (viazi lishe), mihogo iliyoboreshwa, na maharagwe lishe yenye madini chuma kwa wingi. Alisema vyakula hivyo vina virutubishi kama vitamini A, madini ya chuma na zinki ambavyo husaidia kupambana na matatizo ya lishe duni kama vile udumavu, upungufu wa damu, uzito pungufu na utapiamlo.
“Kwa kushirikiana na mdau HarvestPlus, tuligawa kilo 200 za unga wa mahindi lishe katika shule hizo mbili kila moja ikipokea kilo 100. Unga huo ulitumika kupika uji na ugali kwa wanafunzi. Tumeona mwitikio chanya na wanafunzi wameonyesha kufurahia sana aina hiyo ya chakula,” alieleza.
Bi Joyce alihitimisha mkutano kwa kutoa wito kwa serikali na wadau wa lishe kuongeza jitihada za kutoa mbegu bora, mbolea, na kuweka mikakati endelevu ya mpango wa utoaji wa chakula mashuleni ili kusaidia kuboresha mazingira ya kujifunzia.
Halmashauri ya Wilaya Songea
Anuani ya Posta: P.o.box 995, Songea
Simu: 2602320 / 2602176
Simu ya mkononi:
Barua pepe: dedsongea@songeadc.go.tz
Copyright ©2017 songeadc.go.tz. Haki imehifadhiwa