MKUU wa Wilaya ya Songea Mheshimiwa Wilman Kapenjama Ndile amewataka Watendaji wa Kata kuweka msisitizo katika ufuatiliaji na utekelezaji wa afua za lishe.
Ameyasema hayo katika kikao cha robo ya pili cha tathmini ya mkataba wa lishe kilichoudhuriwa na Mwenyekiti wa Halmashauri Mheshimiwa Menas Komba, Mkurugenzi Mtendaji Ndugu Neema Maghembe, wataalamu pamoja na Watendaji wa Kata.
DC Ndile amesema lishe ndio msingi muhimu kwa ustawi wa afya za watoto hivyo amesisitiza wataalamu kuendelea kutoa elimu kwa wazazi juu ya matumizi bora ya lishe ili kuepuka magonjwa yanayosababishwa na lishe duni.
Akizungumza Mwenyekiti wa Halmashauri Mheshimiwa Menas Komba amewasisitiza Watendaji Kata kufanya ufuatiliaji na kuhakikisha shule zote zinatoa chakula na kwa wazazi ambao hawajachangia wachukuliwe hatua.
Kwaupande wake Mkurugenzi Mtendaji Ndugu Neema Maghembe amesema Halmashauri imejipanga vizuri katika suala la kutenga bajeti na kutumia fedha hizo katika kuhakikisha afua za lishe zinatekelezeka.
Akisoma taarifa Afisa Lishe Wilaya Joyce Kamanga amesema Halmashauri imejipanga kuimarisha usimamizi kwenye ngazi ya Kata na Vijiji ambako ndiyo kiini cha kuleta mabadiliko katika jamii kuhusiana na afua za lishe.
Ameongeza kuwa wataongeza wigo katika Kata na Vijiji wa kufanya uchunguzi wa hali ya lishe ili kuweza kutambua hali za lishe za watoto wengi zaidi.
Halmashauri ya Wilaya Songea
Anuani ya Posta: P.o.box 995, Songea
Simu: 2602320 / 2602176
Simu ya mkononi:
Barua pepe: dedsongea@songeadc.go.tz
Copyright ©2017 songeadc.go.tz. Haki imehifadhiwa