Kamati ya uhamasishaji wa uandikishaji katika daftari la kudumu la kupiga kura kutoka Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), ikiongozwa na Abdulrahman Hatibu, imefanya ziara ya kuhamasisha wananchi katika kata mbalimbali za Halmashauri ya Wilaya ya Songea. Ziara hiyo imelenga kutathmini mwenendo wa uandikishaji na kujionea hali ya mwamko wa wananchi katika kutumia haki yao ya kikatiba ya kupiga kura.
Katika ziara hiyo, Hatibu alieleza kuridhishwa na mwitikio wa wananchi katika kujiandikisha akisema kwamba zoezi limeendelea kwa kasi nzuri. "Ikiwa tupo katikati ya siku za uandikishaji, tayari kata nyingi zimefanikiwa kufikia nusu au hata zaidi ya nusu ya malengo yao," alisema Hatibu huku akionyesha matumaini kuwa malengo yote yatatimia baada muda kuisha.
Hata hivyo, alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa wananchi ambao bado hawajajiandikisha kuchukua hatua haraka kabla ya muda kuisha. “Tumeridhishwa na zoezi la uandikishaji, lakini nitoe wito kwa wale wote ambao hawajajiandikisha kujitokeza kwani muda bado upo, na ni haki yao ya msingi kama raia wa Tanzania,” alisisitiza Hatibu, akihimiza umuhimu wa kila raia kushiriki kwenye mchakato wa uchaguzi.
Ziara hiyo imekuwa ni sehemu ya kampeni kubwa inayosimamiwa na TAMISEMI kuhakikisha wananchi wanapata fursa ya kujiandikisha kwa wingi katika daftari la kudumu la wapiga kura. Kamati hiyo imekuwa ikiendesha mikutano na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kujiandikisha ili kuhakikisha sauti zao zinasikika katika chaguzi zijazo.
Kwa ujumla, uandikishaji umeonekana kupata mwitikio chanya kutoka kwa wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea, hali inayoashiria uelewa mzuri wa haki zao za kidemokrasia na umuhimu wa kushiriki katika uchaguzi ujao.
Halmashauri ya Wilaya Songea
Anuani ya Posta: P.o.box 995, Songea
Simu: 2602320 / 2602176
Simu ya mkononi:
Barua pepe: dedsongea@songeadc.go.tz
Copyright ©2017 songeadc.go.tz. Haki imehifadhiwa