Halmashauri ya Wilaya ya Songea, kupitia Kamati ya Fedha, Uongozi, na Mipango (KFUM) inayoongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri, Mheshimiwa Menans Komba, imefanya ziara yenye lengo la kukagua na kusimamia miradi ya maendeleo inayolenga kuboresha huduma za afya katika zahanati za vijijini. Miradi hii imedhaminiwa kupitia mpango wa Sustainable Rural Supply and Sanitation, ikilenga kuboresha miundombinu ya afya kwa wanawake na watoto.
Katika ziara ya leo, kamati imeweza kushuhudia mafanikio makubwa ya ujenzi na maboresho ya vyumba vya mama na mtoto, vyenye huduma muhimu kama vile chumba vya kujifungulia, maeneo ya kupumzikia, pamoja na miundombinu ya maji safi. Uboreshaji huu unaendana na jitihada za Halmashauri katika kuboresha huduma za afya kwa jamii, hasa kwa makundi nyeti kama vile wanawake wajawazito na watoto wachanga.
Zahanati zilizokaguliwa ni pamoja na Zahanati ya Kijiji cha Mpangula, Kata ya Matimila, Zahanati ya Kijiji cha Liweta, na Zahanati ya Kijiji cha Nakahuga, ambazo zote zimenufaika na kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya kisasa vya mama na mtoto, vyoo, na miundombinu ya maji safi.
Mwenyekiti wa Kamati, Mheshimiwa Menans Komba, amesisitiza kuwa miradi hii ni sehemu ya jitihada za Halmashauri ya Wilaya ya Songea kuimarisha huduma za afya vijijini. Ameeleza kuridhishwa na hatua zilizofikiwa na kutoa pongezi kwa wadau wote waliohusika katika kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa kwa weledi mkubwa. Pamoja na mafanikio yaliyopatikana, tathmini zaidi itaendelea kufanyika ili kuhakikisha miradi yote inakamilika kwa ufanisi na kutoa huduma bora kwa wananchi.
Halmashauri ya Wilaya ya Songea imeendelea kuonyesha dhamira ya dhati ya kuboresha huduma za afya na kuleta maendeleo endelevu kwa jamii.
Halmashauri ya Wilaya Songea
Anuani ya Posta: P.o.box 995, Songea
Simu: 2602320 / 2602176
Simu ya mkononi:
Barua pepe: dedsongea@songeadc.go.tz
Copyright ©2017 songeadc.go.tz. Haki imehifadhiwa