Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama (Mb) Peramiho ameomba wananchi kuanza kujiandaa ili kulifanya zao la Mahindi kuwa zao la biashara kwa siku za usoni.
Waziri ametoa kauli hiyo katika ziara yake katika kata ya Matimila ambapo amefanya Mikutano miwili ya hadhara katika vijiji vya Kikunja na Mpingi vilivyopo Halmashauri ya Wilaya ya Songea Mkoani Ruvuma Leo tarehe 08/07/2024.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu ameendelea kutoa ruzuku ya mbolea, kazi kubwa kwetu wakulima ni kuongeza juhudi katika kilimo na uzalishaji wa mahindi.
Waziri Mhagama amesema, “Mwaka huu Mhe. Rais, ametutafutia masoko Nje ya Nchi, lengo letu ni kuhakikisha siku za karibuni tunafanya zao la mahindi kuwa zao la biashara ili liweze kusaidia wananchi kukuza uchumi na pato la familia.”
Aidha Waziri amewaomba wananchi kuendelea kuweka akiba ya chakula cha familia badala ya kuuza chakula chote ili nchi iendelee kuwa na akiba ya chakula.
Waziri ameelezea wananchi kuhusu fursa ya mikopo yenye masharti nafuu, ambapo amewaasa kutumia wasaa huo kufungua shughuli mbalimbali za uchumi, ikiwemo mashine za kusaga za umeme, na kujikita katika kuwekeza katika viwanda vidogo vidogo vya kuchoma chuma.
“Nishati ya umeme inatakiwa kuwasaidia wananchi kupata mapato na shunguli za kukuza kiuchumi,” alisema Waziri Mhagama
Awali Katibu Tawala wa Wilaya ya Songea Ndg. Mtela Mwapamba amewaambia wananchi kwamba watafanya mikutano ya ujirani mwema kati ya Mkuu wa Wilaya ya Songea na Wilaya ya Namtumbo na Kamati za ulinzi na Usalama ili kutatua migogoro ya Mipaka inayohusianisha wilaya hizo mbili.
Aidha Katibu Tawala amewaahidi wananchi wa kijiji cha Kikunja kwamba Serikali kupitia Afisa Ushirika wa Halmashauri ya Songea , itawasaidia kuanzishwa kwa chama chao cha Ushirika katika Kijiji hicho ambacho hakina (AMCOS) Agricultural Marketing Cooperative Society.
“Kuanzishwa kwa AMCOS itasaidia Serikali kupata mapato hivyo ni jukumu la Watendaji wa Serikali kuhakikisha inasimamia mchakato na kanuni za uanzishwaji wake tangu mwanzoni mpaka ukamilikaji wake na kuhakikisha tunailea,“alisema Ndg. Mwapamba
Halmashauri ya Wilaya Songea
Anuani ya Posta: P.o.box 995, Songea
Simu: 2602320 / 2602176
Simu ya mkononi:
Barua pepe: dedsongea@songeadc.go.tz
Copyright ©2017 songeadc.go.tz. Haki imehifadhiwa