Mkuu wa Wilaya ya Songea, Wilman Kapenjama Ndile, ametoa pongezi kwa timu ya afya na watendaji wa kata kwa juhudi zao katika kuimarisha lishe bora kwa wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea. Ndile ametoa pongezi hizi wakati wa kikao maalum cha lishe kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea, ambacho kilikuwa na lengo la kutathmini upatikanaji wa lishe katika ngazi ya kata.
Katika kikao hicho, Ndile alielezea furaha yake kubwa kutokana na utekelezaji mzuri wa maagizo yake, hasa katika maendeleo ya maharage lishe na mahindi lishe yaliyosambazwa na mdau Harvest Plus Arusha. Mbegu hizi zilisambazwa katika shule tano za msingi na tano za sekondari, lengo likiwa ni kurahisisha upatikanaji wa mbegu za kutosha kwa msimu ujao wa kilimo, hatua inayolenga kuboresha lishe bora kwa wanafunzi.
Mkuu wa Wilaya amesisitiza kuwa ufuatiliaji wa utekelezaji wa maagizo yake umeonyesha matokeo chanya, hasa katika mashamba darasa ya maharage lishe na mahindi lishe yaliyopo katika shule zote zilizopokea mbegu hizo. Alitoa pongezi maalum kwa shule za msingi Nambarapi, Magima, na sekondari ya Namihoro kwa usimamizi bora wa mashamba hayo. Ndile alibainisha kuwa hatua hizi zimechangia kwa kiasi kikubwa kuboresha lishe kwa wanafunzi na kuongeza fursa ya upatikanaji wa mbegu bora kwa msimu ujao wa kilimo.
Kutokana na mafanikio haya, Ndile ametoa maelekezo kwa maafisa elimu wa shule za msingi na sekondari kuandikiwa barua za pongezi kwa usimamizi mzuri. "Tumetoka mbali na sasa tumepiga hatua kubwa sana kwani tulikuwa kwenye sifuri na sasa mwanga umeanza kuonekana," alisema Ndile kwa furaha, akisisitiza kuwa jitihada hizi ni matokeo ya kazi kubwa iliyofanyika kuhakikisha lishe bora kwa wanafunzi inaimarika. Pia amewasisi watendaji wa kata waliohudhuria katika kikao hicho kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kwenye mikutano yao ya hadhara juu ya matumizi sahihi ya lishe ili kuimarisha afya za wananchi.
Kikao hiki pia kimehudhuriwa na wadau mbalimbali wa maendeleo pamoja na viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea, ambao kwa pamoja wamekubaliana kuendeleza juhudi hizi kwa msimu ujao wa kilimo ili kuhakikisha kuwa kila mwanafunzi anapata lishe bora shuleni. Ndile aliendelea kusisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya wadau wa lishe na sekta ya elimu katika kufanikisha malengo haya.
Kwa ujumla, hatua hizi za kuimarisha lishe shuleni zinaonekana kuwa na athari kubwa katika kuboresha afya na maendeleo ya watoto wa shule katika Halmashauri ya Wilaya ya Songea, jambo ambalo linatarajiwa kuleta mabadiliko chanya katika jamii kwa ujumla.
Halmashauri ya Wilaya Songea
Anuani ya Posta: P.o.box 995, Songea
Simu: 2602320 / 2602176
Simu ya mkononi:
Barua pepe: dedsongea@songeadc.go.tz
Copyright ©2017 songeadc.go.tz. Haki imehifadhiwa